Taasisi ya kimataifa kujenga chuo cha lishe Arusha

JUMUIYA ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) inapanga kujenga vyuo viwili kutoka 11 vya sasa kikiwamo chuo cha 12 kitakachojishughulisha na lishe, na chuo cha 13 kitakachohusika na afya ya lishe ya umma na mawasiliano.

Mipango hiyo ni sehemu ya mkakati wa ECSA-HC kushughulikia changamoto za lishe miongoni mwa nchi wanachama wake.

Hayo yamebainishwa jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dk Ntuli Kapologwe wakati wa utiaji saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa Miaka Mitano kati ya ECSA-HC na Mtandao wa Asasi za Kiraia zinazohusika na masuala ya lishe (ESA SUN CSN) Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Dk Kapologwe alisisitiza haja ya kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kuimarisha lishe kwa kuwa ukanda wa ECSA unakabiliwa na mzigo mkubwa wa utapiamlo.

Alisema viwango vya udumavu ni zaidi ya asilimia 30, na upungufu wa damu unaoathiri zaidi ya asilimia 35 ya wasichana.

“ECSA kwa sasa inafanya kazi kupitia modeli ya pamoja na vyuo 11 vinavyotoa elimu maalumu katika ukanda huu wote. Katika majadiliano yetu ya hivi karibuni, tuligundua haja ya kuanzisha chuo cha 12 kinachohusika na lishe pekee, na chuo cha 13 kitakachounganisha afya ya lishe ya jamii na mawasiliano,” alisema.

“Hii ni muhimu ili kufanya ajenda ya lishe ionekane zaidi na yenye athari katika jamii zetu,” alieleza Dk Kapologwe.

Pia, alisema MoU waliyoingia itawezesha mashirika yote mawili kukabiliana na changamoto kuu za lishe kwa kukuza mkakati wa lishe wa kikanda, kuimarisha utawala kutoka ngazi ya kimataifa hadi ya kitaifa, na kuwekeza katika utafiti wa lishe ili kusaidia afua zinazotegemea ushahidi wa vigezo.

Naye Mwenyekiti wa mtandao huo wa asasi za kiraia, Edgar Onyango alibainisha kuwa mtandao huo kwa sasa unafanya kazi katika nchi 15 katika ukanda wa ESA huku akiwa na matumaini ya ushirikiano huo kuleta mabadiliko yenye matokeo.

“MoU hii itaongeza uwezo wetu wa utetezi unaotegemea ushahidi. Bila ushahidi, utetezi unapoteza msingi wake. Kushirikiana na ECSA-HC hutuwezesha kuzalisha, kusambaza, na kutumia ushahidi kushawishi sera na bajeti za kitaifa,” alisema Onyango.

Aliongeza: “Lengo letu kuu ni kumaliza utapiamlo ifikapo 2030. Wakati takwimu za sasa zinaonesha kuwa bado tuna safari ndefu, tuna matumaini kwamba kupitia juhudi za pamoja na shirikishi, tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya utapiamlo kote Mashariki na Kusini mwa Afrika”.

Kwa mujibu wake, MoU hiyo itatumika kama mwongozo wa ushirikiano mzuri kati ya kanda za kiuchumi na mashirika ya kiraia katika vita dhidi ya utapiamlo na masuala yanayohusiana na afya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button