Taasisi ya Uongozi yataka mambo 3 yazingatiwe

TAASISI ya Uongozi imewataka watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma wazingatie mambo matatu katika utendaji, ikiwemo kujitawala mwenyewe kwanza.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Kadari Singo alisema hayo Kibaha mkoani Pwani juzi wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watendaji wakuu wapya 111 wa taasisi za umma walioteuliwa kuanzia mwaka 2022.

Singo alisema kupitia kujitawala mwenyewe, kiongozi aangalie namna ya kuwasiliana na watumishi wake pamoja na mawasiliano baina ya taasisi na taasisi kwa sababu mawasiliano yanajenga heshima na weledi kwa taasisi.

Alisema wakuu wa taasisi wanatakiwa wasijione wao wanajua kila kitu na badala yake wawe wanatenga muda wa kutosha kuwasikiliza watumishi wengine kwani njia hiyo italeta heshima kwa viongozi.

Aidha, Singo aliwataka wakuu wa taasisi wahakikishe wanasimamia na kuunganisha watu katika taasisi zao kwa sababu watu wana tabia mbalimbali katika jamii.

Vilevile alisema ni muhimu kwa wakuu wa taasisi kusimamia taasisi kikamilifu ili kuweka mali na miundombinu ya taasisi husika katika hali ya usalama na amani.

“Lazima utawala wako uende hadi katika kusimamia na kulinda mali za taasisi kama magari yanayotumika ndani ya taasisi na rasilimaliwatu kwa sababu ndio msingi wa maendeleo ya taasisi,” alisema Singo.

Alifafanua usimamizi wa taasisi unaenda mbali zaidi hadi kwenye usimamizi wa majengo ili kuyafanya yadumu kwa muda mrefu na kufikia matarajio yaliyokusudiwa.

Aliwataka wakuu hao wa taasisi waache mazoea kuwa taasisi mambo yake yanaanzia ndani na sio getini. Alisema katika baadhi ya taasisi ufunguaji wa mageti na huduma inayotolewa getini sio rafiki kwa maendeleo ya taasisi.

“Uongozi katika taasisi yoyote lazima ujenge mfumo wa utendaji kazi kitimu, hata mgeni akifika anaona na kujua fika kuwa wafanyakazi wanafanya kazi kitaasisi,” alisema Singo.

Alionesha umuhimu kwa taasisi za umma kupeleka watumishi katika mafunzo akigusia kuwa mafunzo kwa watumishi limekuwa jambo la bahati nasibu.

Aliwakumbusha wakuu wa taasisi kuwa ni vizuri kuwaendeleza watumishi ili kupata ufanisi katika utendaji na kuwakumbusha kuacha kuwaendeleza watumishi ambao hawatakuja kutumia elimu hiyo kwa manufaa ya taasisi

Habari Zifananazo

Back to top button