Taasisi yakabidhi watoto vifaa vya shule

DAR ES SALAAM; Taasisi ya kidini ya Al Ameen Foundation (AIF) ya Kijitonyama, Dar es Salaam, imekabidhi vifaa vya shule kwa watoto Kijiji cha Magoza, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Ghalib Monero amesema shughuli ya ugawaji vifaa hivyo ilifanyika kwenye kijijini hapo Januari 3, 2026 na kuhudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wa madrasa na msikiti Sabera.

“Nikiambatana na baadhi ya wanachama wa Taasisi ya Al Ameen Foundation tumegawa madaftari kwa watoto wetu wa Madrasatul Sabera iliyopo Kijiji cha Magoza, Mkuranga, Pwani,” amesema na kuwataja baadhi ya wazee wa madrasa na msikiti Sabera waliohudhuria tukio hilo kuwa ni Sheikh Kassim Kyuta na Mohamed Mpetuka.
Amsema kukabidhi vifaa hivyo kunafuatia mkakati ulioanzishwa na taasisi yake kwa kuhusisha wadau mbalimbali katika programu maalumu iitwayo Vifaa Shule 2026, ambapo wanachama wa taasisi hiyo huchangia ili kusaidia watoto wakiwemo yatima.

“Tukio kubwa zaidi litafanyika Januari 10, 2026 ofisini kwetu Al Ameen Foundation Kijitonyama, ambapo pia tutatoa vifaa mbalimbali ikiwemo madfatari na kalamu kwa watoto,” amesema Monero na kuongeza kuwa taasisi yake ni ya kidini inayohusika na masuala mbalimbali ya kijamii.



