Taasisi yawezesha wanawake 8,378 mafunzo VETA

DODOMA; Taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania imeanza mkakati wa kuwapa mafunzo ya namna kushiriki zabuni za serikali baada ya kumaliza mfanzo yao ya ujuzi katika vyuo vya ufundi (VETA).
Akizungumza wakati wa Maonesho ya 32 ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi (Nanenane 2025), Katibu wa taasisi hiyo, Hamida Khoja amesema kwa sasa wamekuwa wakitoa fursa kwa wanawake ambao ni wanachama wa Wanawake na Samia Tanzania kuongeza ujuzi wao katika sekta mbalimbali.
Amesema hadi kufikia Agosti mosi mwaka huu, wanawake 8,378 kati ya wanawake zaidi ya 10,000 waliojiandikisha wamepata mafunzo na wengine wanaendelea na mafunzo ya ujuzi katika vyuo vya VETA vipatavyo 40.
Hamida alisema mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.
“Taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania inajumuisha wanawake wa makundi yenye viwango vya elimu tofauti tofauti, wapo wenye shahada za uzamivu (PhD) na wapo ambao hawajasoma kabisa, lakini wanapata mafunzi ya ujuzi na stadi ili kujihusisha na ujasiriamali,” amesema.
Hamida alisema kutokana na mafunzo ya ujuzi ambao wanawake wameyapata kupitia VETA wameweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zinaoneshwa kwenye kanda zote ambazo maonesho ya Nanenane yanafanyika.
Alisema utoaji wa mafunzo umelenga kuwajengea uwezo wanawake hao kushiriki katika ushindani wa zabuni, kwa kuanzia na viongozi wa ngazi ya mikoa.
“Tunaomba kila anayehitimu mafunzo ya VETA kabla ya kutoka apewe elimu ya PPRA ya kujiunga kwenye mfumo wa manunuzi na namna ya kuwaomba kazi za serikali na kushiriki kwenye zabuni kulingana na fani yao, mfano kama ni wapishi, au shughuli zingine.
“Taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania imeasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule akiwa Geita na sasa imeenea nchi nzima, kiongozi huyo aliona baada ya kuendelea kuelezea kazi zilizofanywa na Rais Samia basi pia wajengewe ujuzi ili wawe wajasiriamali akaenda kuzungumza na uongozi wa VETA na wazo hili likafika kwa Rais.
“Kwa hiyo tunasema mafunzo haya yanatolewa bure, lakini ukweli ni kwamba yanagramiwa na Mheshimwa Rais, mfano sisi tuliwahi kutaka tuwafundishe wanawake kutengeneza batiki lakini tulishindwa kutokana na gharama za malighafi na fedha ya kumlipa mkufunzi, lakini sasa mafunzo haya anayeshiriki hachangii kwasababu yamegharamiwa na ndio maana walimu wanalipwa na serikali na vifaa vya kufundishia vipo na hakuna chuo kimekwama.”
Hamida alisema mara baada ya kuhitimu mafunzo ya ujuzi yanayotolewa na VETA, tunawashauri wanawake wajiunge kwenye vikundi kulingana na fani zao ili kuweza kunufaika na fursa za sekta ya ugavi na ununuzi.
Taasisi ya Wanawake na Samia ina wanachama katika mikoa yote nchini, na inalenga kuendelea kuwahamasisha wanawake kutumia elimu na ujuzi walioupata kuboresha maisha yao na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi