Taasisi za fedha zawageukia wachimba madini

KATIKA kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wachimbaji wadogo wa madini taasisi za fedha zimeshauri kuundwa kikosi kazi kwa lengo la kuandaa miongozo ya ukopeshaji kwa wachimbaji hao.

Taasisi hizo zimependekeza kuwa  Wizara ya Madini kuandaa miongozo hiyo kwa kushirikiana na taasisi kama Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Vyuo Vikuu na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA).

Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mabenki Nchini (TBA) Abdul Said Msombe amesema wachimbaji wadogo nchini wanapaswa kuzingatia masuala kadhaa ya msingi ambayo yatawawezesha kukopa katika mabenki na kuyataja baadhi kuwa ni pamoja utunzaji wa kumbukumbu za manunuzi na matumizi, kuwa na akaunti katika benki ili kuzirahisishia benki kutoa mikopo.

Msombe ameyataja mengine kuwa ni pamoja na kuhakikisha wanakua na mfumo mzuri wa uendeshaji, kufuata taratibu za kiserikali ikiwemo usajili ili kufahamika kisheria pamoja na kuwa na taarifa zinazoonesha mikataba wanayoingia ikiwemo ya mahali wanaponunua madini, mahali wanapopata huduma, kuzingatia masuala ya kuingia mikataba na watoa huduma mbalimbali.

Msombe ameyasema hayo wakati chama hicho na wawakilishi kutoka benki mbalimbali nchini zikiwemo CRDB, NMB, Azania benki na NBC walipotoa mada kuhusu namna benki hizo zinavyoweza kufanya kazi katika sekta ya Madini hususan kushirikiana na wachimbaji wadogo katika mkutano wa wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa madini ya wiwandani uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na Chama Cha Wachimbaji Madini Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI)

 

Katika hatua nyingine, Msombe amesema kutokana na Sekta ya Madini kuwa ngeni katika shughuli za kibenki, amesema nguvu kubwa inayowekwa na taasisi hizo hivi sasa ni kutoa mikopo katika hatua ya uzalishaji wa madini hayo ikiwemo mikopo ya vifaa.

 

Aidha, taasisi hizo zimeiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa mabenki nchini kuhusu shughuli za sekta ya madini ili kuziwezesha kupata ufahamu na uelewa wa kutosha kuhusu biashara ya madini kuziwezesha kutoa mikopo kwa wachimbaji ili pande zote ziweze kunufaika kikamilifu.

Habari Zifananazo

Back to top button