Taboa yashukuru ruksa safari za usiku

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimeipongeza serikali kwa kuruhusu huduma za usafiri wa mabasi kutolewa kwa saa 24.

Mweka Hazina wa Taboa ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Usalama Barabarani la Taifa, Issa Nkya alisema uamuzi huo utasaidia kukuza uchumi kama ilivyo kwa mataifa mengine.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio chetu cha muda mrefu kwa kuturuhusu kutoa huduma za usafiri kwa saa 24, ukweli kama nchi tulichelewa kutoa huduma hiyo kutokana na kuwa na manufaa mengi hasa katika eneo zima la kukuza uchumi wetu,” alisema Nkya.

Alisema wasafirishaji wanaona kwa usafiri kwa saa 24 kutasaidia kuchagiza ukuaji wa maendeleo ya nchi katika sekta zote kutokana na ukweli kuwa sekta ya usafirishaji ni kiungo kikuu cha kufanikisha maendeleo ya sekta nyingine.

Alitoa mfano kuwa wiki chache tangu huduma za mabasi yaanze kutolewa kwa ratiba inayoanzia saa 9 usiku, wasafiri wanaokwenda mikoa mbalimbali nchini na hata nje ya nchi wametekeleza majukumu yao kwa wakati na kuwahi kurejea katika maeneo yao ndani ya muda.

“Aidha, pamoja na shukrani zetu kwa Rais Samia, sisi kama wasafirishaji pia tunapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kwa kulisimamia suala hadi leo hii tulipofika hapa, ukweli tunawashukuru sana viongozi wetu hawa kwa kuzingatia maslahi ya taifa,” alisema Nkya.

Msemaji wa Taboa, Hashemu Mwalongo pamoja na pongezi, aliiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kutoa ratiba za mabasi hayo ili mabasi yasafiri nyakati tofauti ndani ya saa 24, hatua aliyosisitiza kuwa kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza tabia ya madereva kukimbizana.

Mwalongo alisema wamiliki wa mabasi wanaamini kama Latra itatoa ratiba ya saa 24, pia itawapa mwanya mpana abiria kuchagua muda wa kusafiri kufika maeneo wanayoyataka katika muda wanaoona unawafaa, jambo ambalo pia kwa namna moja au nyingine litaondoa usumbufu kwao

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button