Tahadhari zichukuliwe kukabiliana na kipupwe

JANA Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha kipupwe kinachotarajiwa kuanza Juni hadi Agosti mwaka huu.

Katika utabiri huo TMA ilisema kwa kawaida katika miezi hiyo hali ya baridi na upepo mkali hutawala maeneo mengi nchini na mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi hicho kwa mwaka huu unaonesha kutakuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto katika maeneo mengi ya nchi ingawa yapo yatakayopokea baridi kali.

Kwa mujibu wa TMA, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida na maeneo ya Magharibi mwa Mkoa wa Dodoma.

Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa zaidi Julai huku vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, mwambao wa pwani na visiwa vya Unguja na Pemba.

TMA ilisema kipindi hicho pia kitatawaliwa na hali ya upepo wa wastani unaotarajiwa kuvuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususani katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025, katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

Kwa mujibu wa TMA mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu kutakuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto na kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 na 18 hali inayotarajiwa pia katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma.

Aidha, kwa upande wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba, TMA ilisema hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi.

Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 16 na 24 kwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani, na kati ya nyuzi joto 12 na 20 katika maeneo ya nchi kavu.

Tunaipongeza TMA kwa kutoa taarifa hiyo mapema kwani wananchi watapata muda wa kufanya maandalizi ya kukabiliana na hali yoyote itakayosababishwa na kipupwe hicho.

Tunashauri wananchi kuchukua tahadhari mapema kujikinga na magonjwa yanayotokana na hali hiyo.

Magonjwa hayo ni ya mfumo wa hewa kama pumu, magonjwa ya viungo, homa ya mapafu, magonjwa ya mifugo na ya macho yanayotokana na vumbi linalosababishwa na upepo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button