Takukuru kuchunguza vyama kutolipa wakulima
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Chrisitina Mndeme ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo kuchunguza vyama vya msingi 12 ambavyo vimeshindwa kuwalipa wakulima zaidi ya 900 kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Pia ametoa wiki moja kuhakikisha makampuni mawili ya Mkwawa na Voedsel ambayo yalifunga mkataba na wakulima kwenye ununuaji wa zao la tumbaku ambapo wamepitiliza miezi minne bila kuwalipa wakulima.
RC Mndeme amesema hayo jana wilayani Kahama alipokuwa akiongea na viongozi wa chama kikuu cha ushirika wilayani humo (Kacu) na baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi.
“Vyama hivyo ni Kangeme, Kasela, Mbuni, Twiga Mapamba, Mihama Kabanga Mtakuja Iringabalimi, Nyakashatara, Kimumwe vimeshindwa kurejesha fedha kwenye mabenki kwa asilimia 100 waliyokopa nakushindwa kuwalipa wakulima”alisema Mndeme.
Mndeme alisema ilifanyika biashara huria isiyokuwa na uangalizi mzuri na imeonekana kuwatesa wakulima na kutopata haki hivyo mkuu wa wilaya alisimamie hili na waliohusika kusababisha hasara kwenye benki na wakulima wahojiwe .
“Atakaye bainika kusababisha hasara hiyo achukuliwe hatua ya kufikishwa mahakamani na hakuna chama kitakachoanzishwa kipya bali vyama hivyo vifufuliwe upya hatuwezi kukubali Sh biloni 2.5 zipotee bure,”alisema Mndeme.
Mndeme alisema kampuni ya Mkwawa na Voedsel wanazonunua tumbaku alitaka kufikia tarehe 22 ,Septemba iwe mwisho wawe wamekwisha walipa wakulima wote kwa asilimia 100 kiasi wanachodai zaidi ya dola Millioni 9.5.
Mndeme alisema zao la tumbaku msimu wa 2022/2023 wamefanikiwa kuuza na kuzalisha zaidi ya kilo Millioni 14.38 yenye thamani zaidi ya Sh bilioni 90 na kutaka mkataba wa wakulima na makampuni baadhi ya vipengele viangaliwe upya ili mkulima anufaike.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga Hilda Boniface alisema vyama 12 vinadaiwa na mabenki nakusababisha vyama hivyo kufa kutokana na kutokopesheka tena pia wapo wakulima wanadai kwenye makampuni ambayo wameyauzia tumbaku.
“Changamoto iliyokuwepo wakulima kwenye vyama hivyo wamekuwa wakitorosha tumbaku kwenda kujisajili kwenye vyama vingine ambavyo havidaiwi nakubadili jina huku deni la vyama walivyotoka linakuwa palepale”alisema Boniface.