Takwimu NBS chachu uwekezaji Manyara

MANYARA: TAKWIMU rasmi zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zina umuhimu mkubwa katika kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, huku zikisaidia pia kutambua maeneo yenye fursa za uwekezaji.

Meneja wa Takwimu wa NBS Mkoa wa Manyara, Gidioni Mokiwa, amesema ongezeko la idadi ya watu katika maeneo mbalimbali ni miongoni mwa viashiria vinavyoweza kuchochea shughuli za kiuchumi na kuvutia uwekezaji kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa na huduma.

Mokiwa ameyasema hayo Oktoba 17, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nne ya Biashara ya Tanzanite Kwaraa yanayoendelea wilayani Babati.

Amesema takwimu rasmi zinasaidia kufanya maamuzi sahihi, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango na kuchochea maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa Mokiwa, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ilionesha kuwa Mkoa wa Manyara ulikuwa na idadi ya watu takribani milioni 1.8.

Amesema tangu kufanyika kwa sensa hiyo, idadi ya watu mkoani humo imeendelea kuongezeka na kufikia takribani watu 2,160,000.

“Ukiangalia takwimu za idadi ya watu, zimeendelea kuongezeka. Tangu mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu katika Mkoa wa Manyara imeongezeka na kufikia milioni 2,160,000,” amesema Mokiwa.

Ameeleza kuwa ongezeko hilo linaweza kuwa na manufaa katika kuchochea shughuli za kiuchumi, kwa kuwa linaongeza mahitaji ya bidhaa na huduma na hivyo kufungua fursa katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, biashara na madini.

Amesema matumizi sahihi ya takwimu yanawezesha serikali, wawekezaji na wadau wengine kutambua mahitaji ya wananchi na maeneo yenye fursa, hatua inayoweza kusaidia kupanga uwekezaji unaokidhi mahitaji halisi ya jamii.

‎
‎
‎
‎

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button