TAMISEMI, USAID PS3+ watoa mafunzo mfumo wa IFTMIS

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma awamu ya pili unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID PS3+) wametoa mafunzo kwa wakufunzi wa kitaifa kuhusu Mfumo wa Ukaguzi na Ufuatiliaji wa Fedha (IFTMIS) kwa mamlaka zote nchini.

IFTMIS ni mfumo wa kidigitali ambao umeundwa na wataalamu wa ndani kutoka USAID PS3+ na Tamisemi kwa lengo la kurahisisha ukaguzi na ufuatiliaji wa mapato na matumizi ya fedha katika mamlaka za serikali za mitaa.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi na Ufuatiliaji wa Fedha Tamisemi, Denis Mbilinyi ameeleza kuwa, mfumo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazingatiwa kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya utoaji wa huduma kwa wananchi na hivyo kukuza utawala bora
nchini.

Advertisement

Mbilinyi ameongeza kuwa mfumo wa IFTMIS utarahisisha kubaini mianya ya upotevu wa fedha katika shughuli za kila siku za uendeshaji wa mamlaka hizo na kwamba hali hiyo itawezesha fedha nyingi kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa hususan utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kutatua kero za wananchi katika sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo.

Mtaalamu kutoka mradi wa USAID PS3+, Abdul Kitula amesema waliona umuhimu wa kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Tamisemi kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa mfumo wa IFTMIS
kuhakikisha watumiaji wana weledi wa kutosha kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa fedha katika mamlaka za serikali za mitaa.

“Kazi yetu kubwa kama Mradi wa USAID PS3+ ni kushirikiana na serikali ya Tanzania kuimarisha mifumo yake ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,’’ amesema Kitula.

Naye, Mkaguzi Mkuu wa Ndani kutoka TAMISEMI, Hamis Mjanja amesema kulingana na mpango kazi uliopo, wakufunzi wanaoandaliwa watakwenda kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo kwa ngazi zote nchi nzima. Alisema kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwenye kanda na yataendeshwa kwa awamu ili kuhakikisha mafunzo yanatolewa kufikia kila kundi kikamilifu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Tamisemi, Erick Kitali ameeleza kuwa mfumo wa IFTMIS ukifanya kazi kama ilivyotarajiwa, mamlaka zote za serikali za mitaa zitaweza kufanyiwa tathimini ya utendaji kazi wake na kasoro zitakazobainika zitafanyiwa kazi kwa wakati.

Kitali amesema kuwa hatua hiyo itapunguza hoja mbalimbali kuhusu ukaguzi na kwamba itasaidia kuboresha hati za ukaguzi kwa ujumla.

Mafunzo hayo yalilenga kuandaa wakufunzi wa kitaifa ambao mara baada ya kujengewa uwezo, watakwenda kutoa mafunzo kwa watumiaji wengine wa mfumo wa IFTMIS ngazi ya Wizara, Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.