OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa maelekezo tisa kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika leo Tanzania Bara.
Uchaguzi huo unasimamiwa na kuratibiwa na Tamisemi baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kutupa shauri lililofunguliwa kupinga kutumika kwa kanuni za mwaka 2024 na pingamizi la uchaguzi kusimamiwa na Tamisemi
Wananchi wa Tanzania Bara wanatarajiwa kupiga kura katika vijiji 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274.
Taarifa kutoka Tamisemi jana ilielekeza vituo vya kupigia kura vifunguliwe saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.
Aidha, wapigakura wanapofika kituoni watatakiwa kujipanga foleni kusubiri kabla ya msimamizi msaidizi kuhakiki jina la mhusika kwenye orodha ya wapigakura wa serikali za mitaa iliyobandikwa kwenye kituo kisha ataingia kituoni.
“Mpiga kura atapatiwa karatasi ya kupigia kura kulingana na idadi ya nafasi zinazogombewa… kura itapigwa kwa namna itakayozingatia usiri,” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, Tamisemi imeleelekeza kuwa mpiga kura atatakiwa kuweka alama ya vema katika jina la mgombea anayemtaka na kura ikishapigwa itakunjwa na kutumbukizwa katika sanduku la kura.
“Baada ya kupiga kura, mpigakura atachovya kidole cha mkono katika kidau cha wino… mpiga kura atatakiwa kuondoka eneo la kwenye kituo cha kupiga kura baada ya kupiga kura,” ilieleza taarifa hiyo.