DAR ES SALAAM; CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na wadau wakiwamo wa Mfuko wa Udhamini Wanawake Tanzania (WFT-T) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),kimewataka waathirika wa rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kijinsia mahala pa kazi kupaza sauti zao ili wapate msaada na haki zao nchini .
Pia wameiomba serikali kulichukulia kwa uzito suala la kuwawajibisha wale wote wanaomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi na kwa wafanyakazi ili kuweza kulinda haki zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 22,2023 Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA ,Rose Reuben amesema tatizo la rushwa ya ngono sio la kunyamaziwa sababu linaua ndoto na kuchelewesha malengo ya wanawake na watoto wa kike nchini.
Amesema kwa muda wa miaka mitano mfululizo TAMWA imetekeleza mradi wake wa kuchapisha habari za uchunguzi juu ya rushwa ya ngono kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo mfuko wa udhamini wanawake Tanzania (WFT-T) ,taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU na wanamtandao wa kupinga ukatili wa kijinsia nchini.
Amesema kila mwaka Novemba 25,wataanza safari ya siku 16 za kupingwa ukatili wa Kijinsia,safari hiyo inawakumbusha kuwa ukatili wa Kijinsia ni mchakato unaofanyiwa kazi kila siku na unaohitaji wenye utashi wa jamii kutekeleza.
“Kwa mwaka huu TAMWA katika kuadhimisha maadhimisho hayo ,tumewekeza kupinga rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi na kwa taaluma yetu kupinga unyanyasaji huo katika vyumba vya habari na wanahabari ikiwamo katika shule za habari,”amesisitza Rose.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Mfuko wa Udhamini Wanawake Tanzania (WFT -T), Rose Marandu amesema rushwa ya ngono imekuwa ikiangusha ndoto za watu wengi ambapo inakuwa inadhalilisha na kuua.
Amesema imekuwa inaleta madhara makubwa kwa jamii na kupelekea watu kukosa amani ambapo kesi zake mara nyingi upelekewa kwenye makosa ya uhujumu uchumi.
Naye Mchunguzi Mkuu wa PCCB, Dorothea Mrema amesema kwa mujibu wa makosa yote yaliyopo katika sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya Mwaka 2007 yapo makosa 24 huku kosa moja pekee ambalo lipo kifungu cha 15 ya kuhonga na kupokea ndilo halipo katika sheria ya uhujumu uchumi lakini mengine yote yapo katika uhujumu uchumi.
“Ni ukweli uhujumu uchumi adhabu yake ni kuanzia miaka 20 na kuendelea na makosa yote ikiwemo rushwa ya ngono yanahusishwa na sheria ya uhujumu uchumi,”alisema.