TANAPA kufadhili vizimba vya samaki kudhibiti uvuvi haramu Ziwa Victoria

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekuja na mpango wa kufadhili mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria kwa jamii ya wakazi wanaoishi jirani na hifadhi ya taifa kisiwa cha Rubondo.

Mradi huo ni sehemu ya makundi matatu ya miradi ambayo inahusisha miradi ya kijamii kama vile shule, zahanati na vifaa tiba, pili ni miradi ya kimazingira, kama vile upandaji miti na vitalu, na kundi la tatu ni miradi ya kiuchumi.

Ofisa Mahusiano wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Grayson Chegere ametoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari wakati wa ziara kwenye kisiwa hicho na kueleza mradi huo ni sehemu ya kudhibiti uvuvi haramu.

SOMA: TANAPA yafungua milango ya wawekezaji Rubondo

Chegere amesema mradi wa vizimba vya samaki umeanza kutekelezwa kwa hatua za awali ambapo mchakato unaendelea kuhakikisha utekelezaji wa mradi kwa ukubwa zaidi kupitia fedha za serikali na wafadhili.

Amesema tayari kuna kizimba kimoja katika kijiji cha Bongela lakini ni mradi ni endelevu ambapo taratibu za kuomba zimewekwa wazi kwenye vijiji vyote ambapo wananchi wanatakiwa wajiunge kwenye vikundi ili wawezeshwe.

“Fursa na pesa zinapopatikana tu tunawasaidia ili waweze kujikwamua sasa na vizimba viweze kuwasaidia wasiweze kuingia eneo la hifadhi” amesema Chegere.

Ameongeza kuwa katika kuwezesha ulinzi shirikishi TANAPA kupitia hifadhi ya kisiwa cha Rubondo imetoa elimu ya uhifadhi kwa walimu wa shule 43 kutoka Geita, Muleba na Chato ikiwemo shule za msingi 34 na sekondari tisa.

“Walimu hawa tumewapa jukumu moja la kuweza kutoa elimu ya uhifadhi kwa wanafunzi wa darasa la tano, na kidato cha pili lengo ni kufanya kizazi hiki kiweze kupata elimu ya uhifadhi”, amesema.

Ofisa Mahusiano wa TANAPA, Christine Mbena.

Ofisa Mahusiano wa TANAPA, Christine Mbena amesema jambo la kulinda raslimali za maeneo ya hifadhi ni la msingi na linahitaji nguvu ya pamoja kati ya jamii na mamlaka ili kutengeneza umoja na mshikamano zaidi.

Mbena amesema TANAPA imejizatiti kuhakikisha jamii ya watanzania wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi waweze kutoa ushirikiano wa kutosha katika ulinzi wa rasilimali ili kulinda mazingira ya asili na utalii endelevu.

Sehemu ya wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo.

Mkazi wa kijiji cha Kakanji, Christine Bayona ameomba elimu iwe endelevu kwa makundi ya vijana ili kuwaepusha na tabia hatarishi za kufanya shughuli haramu kwenye maeneo ya hifadhi ya ziwa Viktoria.

Jirani wa Kisiwa cha Rubondo, Fikirini Magoti amesema ni vyema vijana wapewe mazingira rafiki kwa vijana kujiajiri kupitia mradi wa vizimba na miradi mingine ili vijana wawe na uhakika wa mapato bila kutegemea uvuvi haramu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button