TANAPA yafungua milango ya wawekezaji Rubondo

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limefungua milango ya uwekezaji kwenye Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita ili kupanua wigo wa fursa na mapato katika sekta ya utalii nchini.

TANAPA imeweka wazi kuwa juhudi hizo zinakuja kufuatia ongezeko la idadi ya watalii katika hifadhi hiyo ambapo ndani ya kipindi cha miaka minne (2021-2025) kumekuwa na ongezeko la watalii kwa takribani asilimia 78.

Ofisa Uhifadhi daraja la kwanza katika kisiwa cha Rubondo, Bruno Felix ametoa taarifa hiyo katika mahojiano maalum na waandishi na kueleza TANAPA imetenga takribani hekari 5 maalum kwa ajili ya wawekezaji.

Amesema TANAPA imetoa nafasi kwa wawekezaji binafsi kuongeza miundombinu ya huduma ya usafiri, malazi na chakula kwenye hifadhi ya taifa ya Rubondo ili kuendana na ongezeko la watalii kila mwaka.

SOMA: TANAPA yajizatiti kuongeza mazalia ya samaki Ziwa Victoria

Amesema kwa mwaka 2021 wastani wa watalii kwa mwaka ilikuwa 1,100 lakini hadi kufikia mwaka 2025 wastani wa watalii imeongezeka na kufikia 5,000 hali inayoashiria mwitikio mkubwa.

“Mwaka 2021 tulikuwa tunapokea wastani wa watalii wa ndani 1,000 kwa mwaka lakini ukiangalia mpaka sasa hivi (2025) tunapokea wastani wa watalii (wa ndani) 3,000.

“Kwa watalii wa nje takwimu zimeongezeka, mwaka 2021 ilikuwa kipindi cha Corona, tulipokea watalii 106 kutoka nje, lakini ukiangalia ndani ya huu mwaka tunapokea watalii wa nje 2,000”, amesema.

Ofisa Uhifadhi Daraja la Tatu, Zacharia Kimambo.

Naye Ofisa Uhifadhi Daraja la Tatu, Zacharia Kimambo amesema kisiwa cha Rubondo ni miongoni mwa hifadhi ya kipekee yenye mandhari ya kihistoria pamoja na vivutio vya wanyama wa majini na nchi kavu.

Ametaja kivutio kingine kikubwa ni kisiwa cha ndege kilichopo ndani ya hifadhi hiyo ambacho kinatumiwa na ndege kutoka mabara tofauti kama sehemu ya mapumbunziko na eneo maalum la mazalia.

Mkuu wa Mradi wa Kuzoesha Sokwe, Robert Mushi.

Mkuu wa Mradi wa Kuzoesha Sokwe, Robert Mushi amesema sokwe waliopo ndani ya hifadhi hiyo wana utofauti kutokana na kujengewa tabia za mazoea na binadamu tofauti na maeneo mengine.

Ofisa Uhifadhi daraja la Tatu, Amina Said.

Kwa upande wake Ofisa Uhifadhi daraja la Tatu, Amina Said amesema kisiwa cha hifadhi cha Rubondo kina makundi ya ndege zaidi ya 200 ikiwemo wanaohama na wasiohama katika kisiwa hicho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button