Tanapa yaita wawekezaji Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

BODI ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imeendelea kuhamasisha na kuwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika Hifadhi ya Taifa Nyerere ili kukuza utalii katika Ukanda wa Kusini utakaosaidia kuboresha ustawi wa maendeleo kwa jamii.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa uwanja wa ndege Mtemere uliopo ndani ya hifadhi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA na Mkuu wa majeshi mstaafu, Jenerali George Waitara alieleza kuwa bodi imeridhika na kasi ya ukamilishaji wa mradi wa uwanja huo na kuwakaribisha wawekezaji kuchangamkia fursa za kuwekeza katika hifadhi hiyo.

“Tumetembelea mradi huu wa uwanja mdogo wa ndege wa Mtemere unaojengwa kwa Teknolojia ya ‘Polymer’ ambapo upo mbioni kukamilika na majengo ya kupokelea watalii, kuongozea ndege na jengo la zimamoto yamekamilika. Tunawaalika wawekezaji kuja kuwekeza sehemu za malazi ndani ya hifadhi hii ili kukuza utalii wa Kusini mwa Tanzania,” alisema.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya REGROW kwa Bodi ya Wadhamini, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Ephraim Mwangomo ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere alibainisha kuwa kupitia uwanja mpya wa ndege ambao upo asilimia 98 kukamilika, hifadhi inategemea kupokea wageni wengi kwani ndege kubwa na ndogo zitakuwa na uwezo wa kuleta wageni kwa wingi, hivyo kuongeza mapato kwa taifa kupitia sekta ya utalii.

“Kiwanja hiki kitakuwa na uwezo wa kupokea ndege zenye abiria 50 (ATR42) pamoja na ndege ndogo, hali itakayochochea kuongezeka kwa idadi ya watalii na mapato ya serikali yatokanayo na shughuli za uhifadhi na utali,” alieleza. SOMA: TANAPA yaguswa na upungufu wa damu hospitalini

Naye Ofisa Uhifadhi Mkuu na msimamizi wa mradi huo, Michael Joseph alielezea faida ya kutumia teknolojia mpya ya ‘Polymer’ katika kukifanya Kiwanja cha Ndege Mtemere uweze kudumu kwa muda mrefu pamoja na kuendelea kuwa rafiki kwa mazingira asilia.

“Teknolojia ya ‘Polymer’ inayotumika katika ujenzi wa kiwanja kwa kuweka tabaka la juu imara ambapo teknolojia hiyo inasaidia kuondoa vumbi eneo linalotumika kuruka, kutua na maegesho ya ndege hali itakayoboresha na kuimarisha operesheni za ndege ndani ya hifadhi na kusababisha ustawi endelevu na rafiki kwa mazingira na Wanyama,” alifafanua.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button