Tanesco yajizatiti kuongeza umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza jitihada za muda mfupi na za muda wa kati kukabili changamoto ya upungufu wa umeme.

Taarifa ya Tanesco ilieleza jana kuwa jitihada za muda mfupi zilizofanyika ili kuingiza jumla ya megawati 90 ni pamoja na kukamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa LM6000 katika kituo cha Ubungo namba III.

“Aidha, tayari mtambo huu umeshaanza kuingiza megawati 35 za umeme katika Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 25 Novemba kama tulivyoeleza hapo awali; matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kidatu yapo katika hatua za mwisho kukamilika.

“Na tunatarajia mtambo huu utaanza kuingiza megawati 50 za umeme katika Gridi ya Taifa ifikapo tarehe 30 Novemba kama tulivyoeleza hapo awali,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Tanesco makao makuu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa matengenezo katika kituo cha Kinyerezi namba I yamekamilika na kituo kinazalisha umeme katika uwezo wake.

“Majaribio ya mitambo miwili katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I yanaendelea na kwa sasa mitambo hii inaingiza jumla ya megawati 65 za umeme katika Gridi ya Taifa. “Na tunategemea hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba 2022, mitambo hii itakuwa inazalisha jumla ya megawati 90 kama tulivyoeleza hapo awali,” alieleza taarifa hiyo.

Tanesco ilieleza kuwa bado wanaendelea na kazi za matengenezo ya mitambo miwili ya Ubungo namba III na baada ya kukamilika mwishoni mwa Desemba mwaka huu itazalisha megawati 40 za umeme.

Habari Zifananazo

Back to top button