Tanesco yapanda miti 500 vyanzo vya maji Kilolo

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kupitia jukwaa lake la wanawake limeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kupanda miti rafiki na maji zaidi ya 500 katika vyanzo vya maji wilayani Kilolo mkoani Iringa.

Shughuli hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Anne Msolla inalenga kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji ambayo pamoja na matumizi mengine ya kibinadamu ni muhimu kwa uzalishaji wa umeme.

Akishiriki upandaji wa miti hiyo aina ya Mivengi pembezoni mwa Mto Mtitu unaomwaga maji yake Mto Ruaha Mkuu, Msolla aliwataka wananchi wawe mabalozi wazuri katika utunzaji wa miti hiyo akisema ikitunzwa ipasavyo itakuwa sehemu ya ulinzi wa chanzo cha mto huo na mazingira yake.

Awali Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Kilolo, Mhandisi Mwamvita Ally alisema kampeni hiyo ya upandaji miti iliyopewa jina la Panda miti, mvua ndii, umeme ndindindiiiii ina lengo la kupanda miti kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza kwa kishirikiana na halmashauri yao.

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa shirika hilo, Elihuruma Ngowi alisema mabwawa ya kufua umeme kama Mtera, Kihansi, Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani yanategemea sana vyanzo vya maji vya uhakika ili kuzalisha umeme vinginevyo yatashindwa kuzalisha nishati hiyo kwa kiwango chake.

Alisema Mto Ruaha Mkuu ambao mara kwa mara umekuwa ukiathiriwa na shughuli za kibinadamu na kuathiri mtiririko wake wa maji ni moja ya chanzo cha maji cha mradi mpya wa umeme wa Julius Nyerere ambao ujenzi wake umefika asilimia 83.3 hivisasa.

Alisema ili mto huo utiririshe maji yake kwa mwaka mzima kuelekea hadi Bwawa la Mwalimu Nyerere ni lazima vyanzo vyake vikiwemo vya wilayani Kilolo vilindwe.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa shirika hilo, Prisca Maziwa ameishukuru memejimenti ya TANESCO kwa kuwaruhusu kuendesha kampeni hiyo ya upandaji miti ili kuionesha kwa vitendo jamii inayozunguka vyanzo vya maji umuhimu wa kuvitunza kwa maendeleo ya sekta ya nishati ya umeme na Taifa kwa ujuma.

Habari Zifananazo

Back to top button