SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kinatarajiwa kuongezeka kwa wastani wa megawati 220 ifikapo katikati ya Desemba mwaka huu hivyo kupunguza makali ya mgawo wa umeme uliopo kwa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande alisema hatua hiyo imetokana na mikakati inayoendelea kufanywa na shirika hilo kukabili tatizo lililopo.
Chande alisema kwa asilimia kubwa hali ya upungufu wa umeme uliopo nchini umetokana na uwepo wa changamoto ikiwemo ukame na miundombinu ya usambazaji wa umeme.
Akitolea mfano wa changamoto ya miundombinu yake ya usambazaji wa umeme, Chande alisema kwa kituo cha Kihansi kinachozalisha megawati 180 kikiwa na maji kamili, kutokana na hali ya ukame, kwa sasa kinazalisha wastani wa megawati 17 hadi 30, kikipoteza jumla ya megawati 63 kutokana na upungufu huo wa maji.
Pamoja na Kihansi pia alisema kituo cha Pangani ambacho huzalisha megawati 68 kwa sasa kimezimwa kabisa, lakini pia kituo cha Mtera kinachozalisha megawati 80 kwa sasa kinazalisha megawati 75.
Kwa ujumla Chande alisema kiwango cha upungufu wa umeme kilichopo nchini kwa siku hivi sasa ni takribani megawati 300-350 hali inayosababisha uwepo wa mgawo wa umeme.
Alisema kinachofanyika kwa sasa ili kukabiliana na hali hiyo ni uwepo wa juhudi za muda mrefu na mfupi ikiwemo kufanya maboresho ya mashine zake za ufuaji umeme kikiwemo kituo cha Ubungo 3 kinachotarajiwa kuingiza megawati 20 katika Gridi ya Taifa ndani ya siku mbili na zingine 20 mwanzoni mwa Desemba.
Pamoja na kituo hicho pia alisema kituo cha Kidatu chenye uwezo wa kuzalisha megawati 50, matarajio ifikapo wiki ijayo kitaanza kuzalisha umeme ambao utaingizwa katika mfumo.
Pia alisema kituo cha Kinyerezi I, ifikapo mwisho wa mwezi huu kitatoa megawati 90 ambazo zitaingizwa katika mfumo hivyo hivyo kwa pamoja kufanya jumla ya megawati 220 kuingizwa katika Gridi ya Taifa ifikapo katikati ya Desemba.
Alisema kupatikana kwa umeme huo kutawezesha kupungua kwa hali ya uhaba wa umeme uliopo kwa sasa huku akisisitiza kuwa ifikapo Januari jumla ya megawati zingine 90 kutoka Kinyerezi I zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa umeme.