Tanesco yatenga trilioni 4.4/- miradi gridi imara

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema mpaka kufikia mwaka 2035 miradi mingi itakamilika hivyo kutakuwa na gridi imara.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari mkoani Dar es Salaam juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande alisema kufikia mwaka 2030 watakuwa wamemfikia kila mtu na mipango yao ni kukamilisha miradi yote na hapo kutakuwa na gridi imara.

“Miradi kama MrongoKikagati, Kinyerezi 1, bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo Juni 2024 litaanza, pia tunafanya mazungumzo na sekta binafsi, tunazungumza na Total yote hiyo ni baadhi ya miradi yetu.

“Sasa ukishazalisha na kumaliza miradi unapata umeme wa uhakika na bora mwisho tunakwenda kwenye usambazaji ambapo huko kuna changamoto… tumefanya tathmini tumetenga bajeti ya Sh trilioni 4.42 kutatua matatizo ya usambazaji, na katika bajeti iliyopita Rais aliidhinisha shilingi bilioni 500 na tumeshaanza manunuzi tayari wakandarasi wako saiti,” alisema.

Alisema katika kutekeleza hilo mwaka wa kwanza wameanza na Sh trilioni 1.9 na wana miradi ya usambazaji 26 itakayosaidia umeme kutokatika. Kuhusu suala la smart meter (mita janja), Chande alisema wapo karibu kupata za gharama nafuu na huenda wakalikamilisha hilo mwishoni mwa mwaka huu.

“Kwanza nikiri tumechelewa, lakini chelewa ufike, smart meter zipo gharama ni kubwa lakini tunafanya uchunguzi karibu tunakamilisha… unajua smart meter ni mawasiliano kati ya mita na ofisini gharama atahudumia nani? Lakini tunalikamilisha,” alisema.

Akizungumzia nguzo za zege alisema si kwamba hazipo, ila gharama zake ni kubwa na kuongeza kuwa hawajaacha kutumia nguzo za miti bali zitatumika zote. “Unajua nguzo za miti sio mbaya, kuna ambazo zipo tangu miaka ya 70, tukisema tuache kuzitumia kuna watu wanafanya biashara ya hizi nguzo itakuwaje?

Kwa hiyo zinatumika na zile za zege pia zinatumika ingawa ni gharama… utaratibu wetu ni kwamba umeme mdogo utatumia nguzo za miti, ule mkubwa utatumia nguzo za zege,” alisema.

Kuhusu vyura wa kihansi alisema walipelekwa Marekani kuhifadhiwa na wanatarajiwa kurejea nchini Julai mwaka huu. “Vyura walipelekwa Marekani kuhifadhiwa kwa miaka 20, ilitakiwa warudi tangu mwaka juzi lakini kulikuwa na mambo ya Covid ikashindikana, sasa Julai mwaka huu wataanza kurudi. “Sasa watarudishwa wako 500 wamezaliana sana, watarudishwa kwa awamu,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button