Tanga ya nne uchangiaji Pato la Taifa

TANGA; MKUU wa Mkoa wa Tanga, Dk Batlida Burian, amesema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali, sasa mkoa huo umeimarika kiuchumi na unashika nafasi ya nne katika kuchangia pato la taifa.
Amesema hayo wakati akifungua msimu wa nane wa tamasha la Tanga Women Gala, jijini Tanga, ambapo amesema kuwa uwekezaji huo umesisimua uchumi wa Tanga na kuvutia wawekezaji wengi katika sekta mbalimali ikiwamo bandari, viwanda, kilimo, gesi asilia, utalii, uchumi wa buluu na biashara.
“Fursa za kiuchumi zinazidi kufunguka,ambapo hivi karibuni tunakwenda kushuhudia uwekezaji mkubwa wa kiwanda cha nne cha kuzalisha saruji kwenye mkoa wetu,”amesema.

Amesema serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuwawezesha wajasiriamali wadogo kukua, ili kulifikia soko la kimataifa.
Amewaomba wakazi wa Tanga kuendelea kudumisha amani, mshikamano na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili azma ya Rais Dk Samia Suluhusu Hassan kuifanya Tanga kuwa ya viwanda, iweze kupata mafanikio makubwa.

Naye Mkurugenzi wa Tanga Women Gala, Nassoro Makau amesema lengo la taasisi hiyo ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo hususani wanawake kujiimarisha katika shughuli zao ili zikue.
Amesema maonesho ya wajasiriamali ya Tanga Women Gala kwa mwaka huu yatafanyika Septemba 3 hadi 7.



