BODI ya Korosho Nchini (CBT) imeuza korosho ghafi tani 180,483 kwa thamani ya Sh bilioni 693 katika minada 17 ya zao hilo ambayo iliyofanyika ndani ya wiki tatu tangu kufunguliwa kwa msimu wa 2024-2025 Octoba 11, mwaka huu.
Mkurungezi Mkuu wa Bodi hiyo, Francis Alfred amesema hayo leo Oktoba 30, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa masoko na mauzo ya korosho nchini.
Akizungumzia hali ya uzalishaji, Alfred amesema uzalishaji umeongezeka kwa msimu 2024-2025 kulinganisha na msimu uliopita.
“Msimu uliopita mpaka kufikia wiki ya tatu tulikuwa tumeuza tani 60.66, kwa hiyo mtaona kwamba katika msimu wa 2024-2025 katika wiki ya tatu tuna uzalishaji marae tatu ta kile ambacho tulipeleka msimu uliopita,” amesema.
Amesema Sh bilioni 612 kati ya Sh bilioni 693 zimeshalipwa kwa wakulima. Mkurungezi mkuu huyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pembejeo za bure na Kwa wakati kwa wakulima wa Korosho nchini na kuwawezesha kuandaa mashamba Kwa wakati mwaka.