Wananchi wapiga kura serikali za mitaa 2024

DAR ES SALAAM: Mzee Enos SikaongaPanja, mkazi wa Mtaa wa Goba, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, amezishauri mamlaka husika za uchaguzi wa serikali za mitaa kuboresha mpangilio wa upangaji wa majina ya wapiga kura katika daftari la wapiga kura ili kupunguza usumbufu wa utafutaji wa majina.

Akizungumza baada ya zoezi la upigaji kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika nchi nzima isipokuwa Zanzibar, Mzee Panja amesema kwamba licha ya maandalizi mazuri ya uchaguzi wa mwaka 2024, kumekuwepo na changamoto katika upangaji wa majina ya wapiga kura.

Alisema changamoto hii imesababisha usumbufu kwa wapiga kura wakati wa kutafuta majina yao.

Advertisement

“Maandalizi ya uchaguzi yako vizuri lakini mpangilio wa upangaji majina ya wapiga kura haukuwa mzuri, umeleta usumbufu mkubwa,” alisema Mzee Panja.

Aidha, Mzee Panja amewashauri waandaji wa uchaguzi kuzingatia kutumia karatasi za nyeupe badala ya karatasi za rangi ili kuepuka usumbufu kwa watu wenye matatizo ya uoni hafifu.

“Ningejua ningekuja na miwani mingine. Nimepata shida sana kutafuta jina langu kwa sababu makaratasi walionakili orodha ya wapiga kura yalikuwa ya rangi,” aliongeza.

Hata hivyo, wakazi wengine wa Mtaa wa Goba walieleza kuridhika na maandalizi ya uchaguzi.

Happiness Nkali, mmoja wa wapiga kura, alisema: “Mimi nimeona kila kitu kimeenda sawa na kila mtu amechagua mtu anayemtaka.”

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ulifanyika Tanzania Bara pekee, ambapo wananchi walikuwa na fursa ya kuchagua nafasi ya mwenyekiti wa serikali za mitaa na wajumbe.

Jumla ya watanzania 31,282,331 walijiandikisha kupiga kura, sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha wapiga kura 32,987,579.

Idadi hii inaonyesha ongezeko kubwa la idadi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2019, ambapo walijiandikisha wapiga kura 19,681,259, sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha wapiga kura 22,916,412.

SOMA: Rais Samia apiga kura uchaguzi s/mitaa