Tanzania, Canada kushirikiana kukuza ujuzi wadau sekta ya madini

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Ahmed Hussein kuhusu masuala mbalimbali ya kuboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili hasa katika eneo la kuwajengea uwezo wataalamu na wachimbaji wa madini Tanzania katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uchimbaji na uchenjuaji madini.
Mazungumzo hayo yamefanyika Toronto, Canada na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Joseph Sokoine sambamba na wataalamu wa Wizara zote mbili.

Akitoa maelezo ya awali, Waziri Ahmed Hussein ameipongeza Tanzania kwa namna imeweka mazingira mazuri ya ukuaji wa Sekta ya Madini na kwamba Canada itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania hasa katika eneo la kuwajengea uwezo wataalamu na wachimbaji madini kwenye matumizi sahihi ya teknolojia ya uchimbaji na uchenjuaji madini.
“Tumekuwa na miradi ya maendeleo ya elimu nchini Tamzania, hivyo kupitia vyuo vya mafunzo ya Ufundi itakuwa rahisi kuja na mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania, hasa wakina mama na vijana, kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini, “amesema Hussein.

Kwa upande wake, Waziri Anthony Mavunde ameishukuru Canada kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii Tanzania na pia kubainisha uwepo wa kampuni kubwa za Madini kutokea nchi hiyo zimechochea kwa kiwango kikubwa maendeleo ya kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zitokanazo na uwekezaji huo.
“Tanzania hivi sasa tuna programu yenye lengo la kuwezesha ushiriki kamilifu wa wakinamama na vijana kwenye sekta ya madini, hivyo kuwajengea uwezo wa kiujuzi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini kutachochea kukua kwa kasi kwa sekta ya madini,” amesema Mavunde.



