Tanzania, EU kuimarisha biashara, usalama

DAR ES SALAAM; TANZANIA na Umoja wa Ulaya (EU) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kibiashara, utawala bora, demokrasia na ulinzi na usalama wa kikanda na kimataifa.

Wamekubalina hayo Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha majadiliano ya ushirikiano baina ya Tanzania na EU.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi alisema katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara wameeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano chini ya mkataba wa Samoa uliosainiwa mwaka 2023

Chumi alisema pia ushirikiano huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.

Alisema Tanzania inaishukuru EU kwa uwekezaji wa zaidi ya Euro bilioni 720 zilizosaidia utekelezaji wa miradi katika sekta za nishati, uchumi wa buluu, mabadiliko ya tabianchi na mipango ya miji kuwa kijani.

Aidha, Chumi alisema Tanzania imeomba uwekezaji ujao uendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Kuhusu biashara na uwekezaji alisema wamekubaliana kushirikiana kuhakikisha upatikanaji zaidi wa masoko ya bidhaa za Tanzania katika masoko ndani ya EU na kuvutia uwekezaji katika sekta za kimkakati ikiwemo nishati jadidifu na miundombinu.

“Kwa sasa EU imewekeza miradi ya utalii na miundombinu yenye thamani ya Euro bilioni tatu,” alisema Chumi.

Alisema pia wamekubaliana kushirikiana kukabili changamoto za usalama baharini ukiwemo uvuvi haramu na uharamia sambamba na kuangazia nafasi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na mchango wake katika Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kuhusu utawala bora alisema Tanzania imetumia fursa ya ushirikiano huo na akahimiza umuhimu wa utawala bora na demokrasia.

Chumi alisema wamekubaliana kuendelea kuimarisha juhudi za kukabili changamoto za kiusalama za kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya ushirikiano kati ya Tanzania na EU.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa EU anayeshughulikia Kanda ya Afrika katika Kurugenzi ya Huduma za Nje ya Umoja wa Ulaya, Balozi Rita Laranjinha alisema umoja huo utaendelea kushirikiana na Tanzania kutafuta suluhu ya changamoto za kidunia.

Majadiliano ya Tanzania na EU yamefanyika kwa mujibu wa mkataba wa Samoa uliosainiwa mwaka jana unaochukua nafasi ya mkataba wa Cotonou unaoelekeza umuhimu wa kuwa na majadiliano ya mara kwa mara kati ya EU na nchi za Afrika, Caribbean na Pasific.

Habari Zifananazo

Back to top button