Tanzania kupeleka miundombinu ya mawasiliano DRC

Tanzania kupeleka miundombinu ya mawasiliano DRC

SERIKALI ya Tanzania iko tayari kupeleka miundombinu ya mawasiliano katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye,  akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Fursa za Kibiashara na Uwekezaji katika Sekta ya TEHAMA lililoanza leo jijini Lubumbashi.

Kongamano hili linafanyika miezi miwili tu, tangu viongozi wa nchi hizi mbili wakutane hapa DRC, wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Advertisement

“Serikali ya Tanzania iko tayari kuleta miundombinu ya mawasiliano ya Tanzania hususani Mkongo wa Taifa, ili kuiunganisha DRC na nchi jirani.

“Tunaamini katika umoja na ushirikiano wa nchi zetu kushirikiana, ili kufikia malengo ya kiuchumi ya nchi zetu na wananchi wetu kwa ujumla,”  alisema Waziri Nape.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Balozi wa Tanzania nchini  DRC, Said Mshana amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji wa TEHAMA wa DRC kuwa Tanzania ni nchi iliyojipanga kufanya biashara na DRC.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  Dk Jim Yonazi amewataka washiriki wa kongamano hilo kushiriki kwa ukamilifu kwenye majadiliano, ili kuona fursa zilizopo baini ya Tanzania na DRC, ili kubaini maeneo ya ushirikiano na kutumia fursa hizo.

Kongamano hilo ni la kwanza kufanyika baina ya Tanzania na DRC na limeandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Wizara ya Posta na Mawasiliano ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *