Tanzania, Uganda zajadili uimarishaji mpaka

KIKAO cha kamati ya pamoja cha wataalamu  wa Tanzania na Uganda kimeanza mkoani Kagera kujadili uiamarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.

Kikao hicho kimeanza Novemba 5, na kutarajiwa  kumalizika Novemba 7,  na kinafanyika katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa kuhusisha wataalamu kutoka nchi za Tanzania na Uganda.

Advertisement

Akifungua kikao hicho cha siku tatu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kager, Hajat  Fatma Abuubakar Mwasa, katibu Tawala  Mkoa wa Kagera, Stephen Ndaki amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kutekeleza zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo mbili.

Kupitia hotuba hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Ndaki amesema, Tanzania na Uganda zimekuwa na mahusiano mazuri ikiwemo  tamaduni zinazofanana alizozieleza kuwa, zimewezesha wananchi wa nchi hizo mbili kuishi kwa upendo.

Mpaka wa Tanzania na Uganda una urefu wa  takriban km 397.8 ambapo kati ya hizo km109 ni nchi kavu , km 42.8 ni sehemu ya mto kagera  na km 246 ni sehemu ya ziwa victoria.

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika kuwa, ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.