Tanzania, Uganda zasaini uimarishaji mpaka wa kimataifa

TANZANIA na Uganda zimetia saini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yamefikiwa mwisho wa kikao cha Kamati ya Pamoja ya Wataalamu (JTC) kati ya nchi hizo kilichokuwa na lengo la kujadiliana namna ya kuimarisha mpaka wa Tanzania na Uganda.

Utiaji saini makubaliano hayo umefanyika katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Hamdouny Mansour na Mkuu wa ujumbe wa wataalamu kutoka Uganda, Jacqueline Banana Wabyona.

Advertisement

Wakati wa utiaji saini makubaliano hayo, viongozi wote wawili wameonesha kuridhishwa na namna wataalamu wa nchi hizo mbili walivyoshiriki majadiliano ya pande hizo mbili na hatimaye kufanikisha kusainiwa kwa makubaliano hayo.

SOMA: Tanzania, Uganda zajadili uimarishaji mpaka

Kikao cha Kamati ya pamoja cha wataalamu  wa Tanzania na Uganda (JTC) kilianza Novemba 5 mkoani Kagera ambapo kimejadili mambo mbalimbali ha uiamarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.

Mpaka wa Tanzania na Uganda una urefu wa takriban km 397.8 ambapo kati ya hizo km109 ni nchi kavu , km 42.8 ni sehemu ya Mto Kagera  na km 246 ni sehemu ya Ziwa Victoria.

Uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika(AU) kuwa, ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.