RIPOTI mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), inaonesha watoto milioni 67 walikosa chanjo moja au zaidi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita duniani.
Limetaja sababu za changamoto hiyo kuwa ni usumbufu wa huduma unaosababishwa na migogoro na udhaifu wa mifumo, kupungua kwa imani, mifumo duni ya afya na uchache wa rasilimali zilizopo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kumekuwepo na kupungua kwa imani katika chanjo za watoto kwa asilimia hadi 44 katika baadhi ya nchi kutokana na mkanganyiko wa uelewa hasa wakati wa janga la Covid-19.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Dar es Salaam, Aprili 20, mwaka huu, mtazamo wa umma kuhusu umuhimu wa chanjo kwa watoto ulipungua wakati huo katika nchi 52 kati ya 55 zilizofanyiwa utafiti.
Kuhusu hali ya watoto duniani, ripoti hiyo inasema umuhimu wa chanjo kwa watoto ulipungua kwa zaidi ya theluthi moja katika Jamhuri ya Korea, Papua New Guinea, Ghana, Senegal na Japan baada ya kuanza kwa janga hilo.
Katika takwimu hizo mpya zilizokusanywa na The Vaccine Confidence Project na kuchapishwa na Unicef mataifa ya China, India na Mexico pekee ndio zinazoonesha kutotetereka kwa mtazamo wa umuhimu wa chanjo.
“Katika nchi nyingi, watu walio na umri wa chini ya miaka 35 na wanawake walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuripoti imani ndogo kuhusu chanjo kwa watoto baada ya janga hili kuanza,” ilisema ripoti.
Ripoti inashauri utafiti zaidi unatakiwa kufanywa kuona kama majanga ni chanzo kikubwa cha changamoto za chanjo.
Hata hivyo, licha ya changamoto hiyo utafiti umeonesha katika nchi 55 bado imani kwa chanjo ilibaki kwa asilimia 80.
Unicef inasema kuna shaka ya kuendelea kushuka kwa imani kwa chanjo kutokana na kuendelea kuwepo kwa habari zinazopotosha kuhusu chanjo, kupungua kwa uaminifu katika utaalamu na mgawanyiko wa kisiasa.
“Katika kilele cha janga hili, wanasayansi walitengeneza chanjo haraka zilizookoa maisha mengi. Lakini licha ya mafanikio haya ya kihistoria, hofu na taarifa potofu kuhusu aina zote za chanjo zilienea kama vile virusi vyenyewe,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Catherine Russell.
Anataka juhudi ili hofu isizuie watoto kupata kinga dhidi ya surua, diphtheria au magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika.
Kulingana na ripoti hiyo, kati ya wastani wa watoto milioni 67 ambao walikosa kabisa au sehemu ya chanjo ya kawaida kutoka mwaka 2019 hadi 2021, milioni 4.6 kati yao walikuwa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Tanzania pekee, idadi ya watoto waliokosa inafikia 400,000.
Kutokana na changamoto hiyo, Unicef nchini Tanzania inaisaidia na serikali kupitia Wizara ya Afya kuimarisha mfumo wa huduma ya afya ya msingi kukabiliana na suala la dozi sifuri.
Hatua hiyo itazingatia; kutathmini na kubainisha jamii zenye dozi sifuri na kuweka mikakati ya kuwafikia watoto hao; kuhakikisha kunapelekwa kwa wahudumu wa afya katika jamii; mawasiliano yanayolengwa ya mabadiliko ya kijamii na kitabia ambayo huboresha maarifa na mitazamo; na kuongeza uwezo sahihi wa usimamizi na uhifadhi wa chanjo.
“Nina imani kuwa chini ya uongozi bora wa Serikali na Wizara ya Afya, na kwa msaada wa mfumo wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kama vile Unicef na WHO na kwa msaada wa washirika wa maendeleo, tutaona kupungua kwa idadi ya watoto wa dozi sifuri kote nchini,” alisema Shalini Bahuguna, Mwakilishi wa Unicef Tanzania.
Bahuguna alisema watoto waliozaliwa kabla au wakati wa janga hilo sasa wanapita umri ambao kwa kawaida wangechanjwa na kusisitiza hitaji la hatua za haraka ili kuwapata wale ambao walikosa na kuzuia milipuko ya magonjwa.
Kwa mfano mwaka 2022, idadi ya wagonjwa wa surua ilikuwa mara mbili ya mwaka uliopita, idadi ya watoto waliopooza kwa polio iliongezeka kwa asilimia 16 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021.
Unicef inasema kati ya watoto milioni 67 ambao walikosa chanjo ya kawaida kati ya 2019 na 2022, milioni 48 hawakupokea chanjo moja ya kawaida, inayojulikana pia kama “dozi sifuri”.
Kufikia mwisho wa 2021, India na Nigeria zilikuwa na idadi kubwa zaidi ya watoto wasio na dozi sifuri lakini ongezeko la idadi ya watoto walio na dozi sifuri pia lilikuwa nchini Myanmar na Ufilipino.
Ripoti inaeleza watoto wanaokosa nafasi wanaishi katika jamii maskini zaidi, za mbali na zilizotengwa, wakati fulani zilizoathiriwa na migogoro.
Data mpya iliyotolewa na ripoti hiyo na Kituo cha Kimataifa cha Usawa katika Afya iligundua kuwa katika kaya maskini zaidi, mtoto mmoja kati ya watano hana dozi sifuri wakati kwa tajiri zaidi ni mmoja tu kati ya 20.
Aidha, watoto ambao hawajachanjwa mara nyingi huishi katika mazingira magumu na huishi na wanawake waliokosa nafasi kwenda shule na ambao wanapewa nafasi ndogo katika maamuzi ya familia.
Ili kuchanja kila mtoto, ni muhimu kuimarisha huduma ya afya ya msingi na kuwapa wafanyakazi wengi wao wanawake walio mstari wa mbele rasilimali na usaidizi wanaohitaji.
Ripoti inaona wanawake wako mstari wa mbele kutoa chanjo lakini wanakabiliwa na malipo duni, ajira isiyo rasmi, ukosefu wa mafunzo rasmi, kazi na vitisho kwa usalama wao.
Ili kukabiliana na janga hili la maisha ya watoto, Unicef inatoa wito kwa serikali kuunga mkono dhamira yao ya kuongeza ufadhili wa chanjo na kufanya kazi na washikadau kufungua rasilimali zilizopo, ikiwa ni pamoja na fedha zilizobaki za Covid-19, kutekeleza kwa haraka na kuharakisha chanjo ya kuambukizwa na juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya milipuko ya magonjwa.
Ripoti hiyo inazitaka serikali kutambua na kuwafikia watoto wote kwa haraka, hasa wale waliokosa chanjo wakati wa janga la Covid-19 na kuimarisha mahitaji ya chanjo.
Pia kujenga mifumo thabiti ya afya kupitia uwekezaji kwa wahudumu wa afya wanawake, uvumbuzi na utengenezaji wa bidhaa za ndani.
“Chanjo zimeokoa mamilioni ya maisha na kulinda jamii dhidi ya milipuko ya magonjwa hatari,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Catherine Russell.