Tanzania yajipanga kurusha satelaiti

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali inaendelea kutekeleza wa mpango mkakati wa miaka mitano wa anga za juu utakaoiwezesha Tanzania kurusha satelaiti.
Amesema Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam imepata mradi wa utafiti wa urushaji wa satelaiti unaosimamiwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya anga za juu ikishirikiana na Taasisi ya Anga za Juu ya Japan (JAXA).
Waziri Majaliwa amesema hayo leo Oktoba 17, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Kongamano la Nane la Mwaka la Tehama lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
SOMA: Majaliwa atoa maagizo kwa Mamlaka Sekta ya Habari
“Katika eneo hili maandalizi ya utungwaji wa sera, sheria na uridhiwaji wa mikataba ya kimataifa ya masuala ya anga za juu inaendelea,” amesema Majaliwa.
Majaliwa ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kukusanya vijana wabunifu wenye uwezo wa kubuni teknolojia zenye manufaa kwa taifa: “Lakini simamieni hizi tafiti zenye kutoa matokeo na vijana hao waendelee kupewa fursa na kazi hizo ziingie kwa jamii na zianze kutumika.
Ameiagiza Wizara ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari isimamie na kuhakikisha ujenzi wa Vituo vya Ubunifu (Innovation Hubs) katika mikoa iliyokubalika unafanyika kama ilivyopangwa.
Majaliwa ameitaka wizara hiyo ihamasishe matumizi ya Tehama katika kutoa huduma, biashara na uzalishaji ili kuongeza uwazi, ufanisi na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii;
Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ambapo kwa mwaka fedha 2023/24 jumla ya urefu wa kilomita 1,592 za mkongo wa taifa zimejengwa na kufika katika wilaya 83.
“Pia umoja wa watoa huduma za mawasiliano (consortium of telecom operators) wameweza kujenga jumla ya kilomita 2,595 ambazo zinafanya mkongo wa taifa kuwa na kilomita 13,820. Wizara imehamisha shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano na kituo cha kuhifadhia data (NIDC) kwenda katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL)”
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD) Nardos Bekele-Thomas amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha Tanzania inatumia ukuaji wa sekta ya Tehama katika kuchagiza maendeleo endelevu nchini.
View this post on Instagram