Tanzania yang’ara Tehama Afrika

Tanzania yang’ara Tehama Afrika

TANZANIA ni miongoni mwa nchi 10 bora barani Afrika zinazofanywa vizuri katika suala la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kwa  nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni ya pili.

Mchango wa sekta hiyo utokanao na mapato ya kodi ni  asilimia 4.3 na mchango wake kwa Pato la Taifa imepanda kutoka asilimia 1.5 mwaka 2004 hadi  asilimia 2.4 kwa mwaka 2013.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Tehama , Dk Nkundwe Mwasaga, amesema hayo leo Dar  es Salaam, wakati akizungumza na wadau wa teknolojia ya mawasiliano nchini waliokutana kujadili kufikia uchumi wa kidigitali.

Advertisement

Ametolea mfano nchi ya Kenya kuwa mchango wake kwa Pato la Taifa ni asilimia nane na kushauri wadau kutoa michango yenye kuhakikisha uchumi wa  kidigitali inafikiwa, ili kukuza uchumi wa nchi.

Amesema lipo soko  kubwa ambalo halijafikiwa, lenye kuwezesha kufikiwa kwa uchumi wa kidigitali  nchini pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi walio wengi, kutokana na bidhaa wanazozalisha.

Amesema kwa sasa  idadi ya watu kwa nchi za EAC ni milioni 174, wanaochangia Pato la Taifa katika Kanda zao ukifikia Dola bilioni 163 na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), wapo watu milioni 344 wakifikia mchango wa Dola za Marekani  bilioni 720, soko ambalo halijafikiwa ipasavyo.

Hata hivyo amesema ipo haja ya kuwa na sera na taratibu zinazowiana katika nchi husika, ili kufikiwa kwa uchumi wa kidigitali na kuwa na mazingira yanayoruhusu mabadiliko na kupata ujuzi wa kidigitali.

” Tumekutana tujadiliane  na wadau kwa kuwa nchi nyingi  zimefikia  katika hatua  nzuri na sisi pia tuweze kukabiliana na kuona ni kwa jinsi gani ya kufikia mabadiliko ya uchumi wa kidigitali,” amesema na kuongeza kuwa Watanzania wasiwe watumishi wa mitandao ya wengine ni vyema kuongeza  ubunifu  na sekta ya Tehama iwe na mchango kwa vijana na ajira.

Amesema suala la uchumi wa kidigitali inawagusa Watanzania wote, waangalie jinsi ya kusaidia Watanzania kupata ujuzi wa msingi na kufanya shughuli zao za kibiashara na kutumia kama fursa katika mitandao kuangalia mifumo ya mawasiliano ya kidigitali,.