Tanzania yazidi kuwavutia wawekezaji kimataifa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ushirikiano wa Tanzania na Japan umezidi kukua na kuimarika katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia ambapo mauzo ya biashara kati ya nchi hizo yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni saba mwaka 2023 hadi Dola bilioni 37 kwa mwaka 2024.

Majaliwa aliyasema hayo jana alipomwakilisha, Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan.

Alisema Wajapan wanapenda sana bidhaa kutoka Tanzania zikiwemo za kilimo kama chai, kahawa, ufuta, tumbaku, tingatinga, vinyago, katani, viungo kama karafuu pamoja na madini yanayopatikana nchini.

Kiongozi huyo, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na duniani kote waje kuwekeza katika maeneo kama elimu, afya, miundombinu, nishati, kilimo, utalii kwani Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na pia ina amani na utulivu.

“…Tanzania licha ya kuwa na fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi yenye rutuba, amani na mazingira tulivu, pia ni kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa kuwa inapakana na nchi saba ambazo ni Uganda, Rwanda, Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Zambia, Malawi na Msumbuji hivyo kuwawezesha wawekezaji kupata masoko ya uhakika katika mataifa hayo,” alisema.

Alisema serikali ipo katika mchakato wa kuvifanyia maboresho viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Nyerere maarufu Sabasaba ili viwe na hadhi ya kimataifa na kuwezesha kufanyika mikutano na maonesho ya biashara ya kikanda na kimataifa.

Monesho hayo yamehudhuriwa na viongozi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Maonesho hayo yalianza tangu Aprili 13, 2025 na yanatarajia kumalizika Oktoba 13, 2025, hii ni mara ya pili kwa Japan (Osaka) kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ya kimataifa, ambapo mara ya mwisho yalifanyika 1970 (EXPO 1970).

Leo, Majaliwa anatarajiwa kushiriki kongamano la biashara, uwekezaji na utalii litakalohusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Japan.

Pia, Majaliwa atashiriki katika mikutano ya uwili na viongozi wa Serikali ya Japan, mashirika ya maendeleo na watendaji wakuu wa kampuni mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button