TASWA Media Day Bonanza Des.9
DAR ES SALAAM; TAMASHA maalum kwa ajili ya wadau mbalimbali kutoka vyombo vya habari ‘TASWA Media Day Bonanza’ linatarajiwa kufanyika Desemba 9, 2023.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa TASWA, Alfred Lucas imesema lengo la bonanza hilo linaloandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ni kuwaweka pamoja kubadilishana mawazo na kufurahi, waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari.
“TASWA miaka ya nyuma ilikuwa kila mwaka inakutanisha pamoja wanahabari katika Media Day Bonanza, lakini miaka ya karibuni haikufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali.
“Uongozi wa TASWA ulioingia madarakani mapema mwaka huu kwa kuona umuhimu wa jambo hilo umelifanyia kazi na kuzungumza na wadau mbalimbali ambao tayari wameafiki kudhamini bonanza hilo na tupo hatua za mwisho za mazungumzo yetu.
“TASWA inaamini bonanza hilo litakalofanyika Dar es Salaam litakata kiu ya wanahabari ambao kwa miaka mingi hawajakaa pamoja na kubadilishana mawazo. Utaratibu mzima wa bonanza hilo ikiwemo kupata uwakilishi wa baadhi ya wanahabari kutoka mikoani unafanyiwa kazi,” imesema taarifa ya Lucas.