TASWA Mwambao Marathon kufanyika Tanga

DAR ES SALAAM; Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), mashindano ya riadha yajulikanayo kama ‘ TASWA Mwambao Marathon 2024’ yatakayofanyika Septemba 29, 2024 jijini Tanga.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa TASWA, Imani Makongoro imesema mbio hizo ni maalumu kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, ili kutunza mazingira na kumtua mama kuni kichwani.

“Dhamira ya TASWA ni kushiriki kusukuma mbele Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutaka hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia.

“Uhamasishaji utaanzia jijini Tanga na baadaye mikoa mingine itafuata kwa mpangilio utakaotangazwa wakati wa kutambulisha rasmi mbio hizo hivi karibuni.

“Tunakaribisha mashirika ya ndani na nje, taasisi, kampuni, watu binafsi, wadau wa mazingira na nishati safi ya kupikia, kushirikiana nasi kufanikisha mbio hizo ambazo ni Kilometa 21, KM 10 na mbio za kujifurahisha (Fun Run) za KM 5. TASWA inashukuru uongozi wa Riadha Tanzania (RT) kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia kuhusu jambo hilo,” imesema taarifa hiyo.

Wakati huohuo, Makongoro amesema Mkutano Mkuu wa mwaka wa TASWA unatarajiwa kufanyika jijini Tanga, Septemba 28, 2024.

“Pamoja na ajenda za kawaida zilizopo kwenye katiba, kutafanyika kuhusu nafasi ya wanahabari kuelekea Afcon 2027.Washiriki wa mkutano huo ni wanachama wote wa TASWA wa zamani na wapya, wataokuwa wamelipia ada ya uanachama. Baada ya mkutano wanachama wetu watatembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria mkoani Tanga. Mwisho wa kuthibitisha kushiriki na kulipia ada ya mwaka mmoja ni Agosti 30, 2024,” amesema Makongoro.

Pia amesema mkutano huo utatumika kufanya uzinduzi wa programu maalumu ya mafunzo kwa ajili ya waandishi wa habari za michezo chipukizi (TASWA Young Reporters Programme) iliyotangazwa Mei mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button