‘Tatizo vijana tunapigana shoti wenyewe’

IRINGA; NAIBU Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amezungumzia jinsi “majungu” yanavyowatafuna vijana wengi hususani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wenye sifa za uongozi, akisema yameendelea kuua matumaini yao ya ndoto zao za kimaisha.

Amesema hayo mjini Iringa wakati akifungua mahafali ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) seneti ya vyuo na vyuo vikuu vya mkoa wa Iringa.

“Shida ya vijana wa CCM tunawaza kupigana shoti (majungu), asubuhi hadi jioni,  kwa sababu tunaumizwa sana na mafanikio au maendeleo ya watu au vijana wenzetu tunaowafahamu. Huu umekuwa ugonjwa mbaya na sugu kwa Watanzania,” amesema.

Advertisement

Kihenzile aliyetangazwa kuwa mlezi wa seneti hiyo mkoa wa Iringa,  amesema matokeo ya majungu hayo yamewafanya wengi wanaoyapiga na wanaopigwa kushindwa kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za maisha yao.

Amewataka vijana wa Iringa kuonesha tofauti kwa kueleza mazuri zaidi ya vijana wenzao, badala ya mabaya yao akisema; “Tujenge moyo wa kupendana, kuheshimiana na kushikamana ili kila mmoja awe na kesho yake nzuri.”

Ameipongeza Tanzania akisema ina mfumo mzuri unaoweza kumuwezesha mtu yoyote akiwemo anayetoka katika familia masikini kuwa kiongozi katika ngazi yoyote.

Akitoa mfano wa jinsi yeye mwenyewe kama mtoto wa masikini alivyopitia hatua mbalimbali hadi kufikia ngazi ya Naibu Waziri, Kihenzile amesema mwaka 2008 alijiunga UVCCM na uvumilivu wake wa hadi mwaka 2016 ulimuwezesha kuteuliuwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha (DAS).

“Aidha nimekuwa Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kabla ya mwaka 2020 kwenda nyumbani Mufindi na kugombea ubunge na kushinda kabla wabunge wenzangu hawajanichagua kuwa mwenyekiti wa bunge na baadae Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuniteua kuwa Naibu waziri,” amesema.