TAWA yatoa Sh bilioni 9.6 kama gawio kwa vijiji

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imetoa  Sh bilioni 9.6 kwa Halmashauri na Vijiji vilivyopo pembezoni mwa mapori ya akiba na mapori tengefu zitokanazo na asilimia 25 ya ada ya wanyamapori waliowindwa na utalii wa picha kwa kipindi cha kuanzia Aprili 2022 hadi  Desemba 2022.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Mabula Misungwi Nyanda amesema hayo Mei 10, 2023 akiwa kwenye  Ofisi ya Pori la Akiba Kizigo, Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida,  akizungumza na watumishi wakati wa kikazi ya kikazi  Kanda ya Kati.

Nyanda amesema uwindaji wa kitalii unaofanyika katika mapori ya akiba na mapori tengefu yanayosimamiwa na mamlaka hiyo umechangia kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi  wa Taifa.

Amesema umechangia kukuza uchunmi kwa  mwananchi mmoja mmoja hususan wale waishio pembezoni mwa mapori hayo.

Hivyo ameupongeza uongozi wa pori hilo na kanda kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwahimiza  kuongeza ubunifu, bidii ya kazi ili  kuongeza mapato ya Mamlaka  na hivyo kuchangia katika pato la Taifa.

“Kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha tuhakikishe tunafanya kazi kwa kujituma, kwa bidii ili kurudisha shukrani kwa Serikali kwa namna inavyotujali” amesema  Kamishna  Nyanda

Nyanda amewaagiza   viongozi na Watumishi wa Kanda  hiyo  kuhakikisha Vitalu vyote vya Uwindaji wa Kitalii katika Pori la Akiba Kizigo vinapata wawekezaji ikizingatiwa kuwa Pori hilo lina jumla ya Vitalu vinne vya Uwindaji ambapo viwili kati ya vinne vimepata wawekezaji.

Kwa wanyamapori wakali na waharibifu amesema mkazo wa Wizara na Taasisi (TAWA) ni kuhakikisha kuwa adha wanayoipata wananchi kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu inadhibitiwa kikamilifu.

“Hili suala la wanyamapori wakali na waharibifu ni la kupambana nalo usiku na mchana, tupambane kwa nguvu zote na tufanye kila linalowezekana kuhakikisha linadhibitiwa” amesisitiza Kamishna Nyanda

Nyanda  amesisitiza  suala la viongozi wa vijiji, kata na wilaya kupatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya matumizi bora ya ardhi kwani wao ndio huwapatia wananchi vibali vya ujenzi na makazi.

Kamishna Nyanda amesema  kutokana na  kutoelewa huko,  wananchi huanzisha kilimo na makazi  holela na hivyo kuvamiwa na wanyamapori wakali wakiwemo Tembo.

Nyanda ameelekeza  watumishi wa pori hilo  kuimarisha mashirikiano na Wadau wa Uhifadhi ili  kujenga  mahusiano mazuri na kufanya kazi kwa kushirikiana na Wananchi wote wanaozunguka hifadhi hiyo, kwa kufanya hivyo watajenga taswira nzuri ya Taasisi kwa Umma.

Habari Zifananazo

Back to top button