TBC, WildAid wahimiza uhifadhi mazingira

DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Utangazaji Tanzania (TBC), kupitia mpango wake maalum wa uhifadhi wa mazingira unaorushwa kupitia Tanzania Safari Channel, limetoa wito kwa Watanzania wote kuwajibika katika kuyahifadhi mazingira ya nchi.

Wito huo umetolewa Dar es Salaam leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Daphrosa Kimbory katika uzinduzi wa kampeni ya Mimi ni Mhifadhi inayoungwa mkono pia na Community Wildlife Management Areas Consortium (CWMAC), Honeyguide Foundation na WildAid.

Kimbory, amesema kuwa jukumu la kulinda misitu, rasilimali za asili na mazingira kwa ujumla ni la kila Mtanzania, na TBC kama chombo cha taifa cha habari kina wajibu wa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha.

“Uhifadhi wa mazingira ni jukumu letu sote,” alisema Kimbory. “TBC inatambua umuhimu wa kulinda mifumo ya ikolojia ya asili. Tunatumia majukwaa yetu yote kuwahamasisha na kuwahimiza Watanzania wachukue hatua bila kujali nafasi au hadhi yao katika jamii.”

Kimbory pia alielezea namna TBC inavyoshiriki kwenye kampeni za upandaji miti, hasa kupitia mpango wa ‘27 ya Kijani’ uliozinduliwa Januari 2023 kwa heshima ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kampeni hiyo ilihamasisha upandaji wa miti kuanzia Januari 1 hadi 27 katika maeneo mbalimbali, ikiwemo shule na kambi za jeshi, ikiwa ni njia ya kumuenzi Rais.

Kwa mujibu wa Kimbory, kwa ushauri wa Dk Ayubu Rioba, kampeni hiyo haikuishia kwenye tukio hilo la Januari, bali imeendelea hadi leo, kila tarehe 27 ya mwezi.

Nakaaya Sumari, mtangazaji wa Tanzania Safari Channel na balozi wa shirika la kimataifa la Wild Aid, alisema:

“Mazingira ndiyo yanayotoa rutuba ya ardhi yetu, bahari safi, mandhari ya kuvutia na rasilimali tunazotegemea kwa maisha ya kila siku. Tanzania ina idadi kubwa zaidi ya simba duniani na inashika nafasi ya pili kwa idadi ya tembo.”

Nakaaya alibainisha kuwa utalii unaotegemea mazingira unachangia takribani asilimia 18 ya pato la taifa (GDP) na kutoa ajira zaidi ya milioni 1.5 kila mwaka, huku mapato yake yakiwanufaisha moja kwa moja wananchi wa vijijini kupitia uboreshaji wa shule, vituo vya afya na miundombinu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button