TFF yakabidhi mipira shule za msingi Simiyu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekabidhi mipira 1,000 kwa shule za msingi 34 katika wa Mkoa wa Simiyu kwa lengo la kutekeleza programu za michezo shuleni.

Programu hiyo imeanzishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ikiwa ni mbadala wa programu ya grassroot ambapo lengo lake ni kukuza vipaji kwa wanafunzi.

Akizungumza katika hafla leo ya kukabidi mipira hiyo kwa niaba ya Rais wa TFF, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Mkoa huo (SIFA) Osuri Kosuri amesema Mkoa wa Simiyu umekuwa mnufaka wa mipira hiyo kati ya mikoa 14 Tanzania Bara na Zanzibar.

Advertisement

Kosuri ameeleza kuwa jumla ya shule 34 kwa mkoa huo zitapatiwa mipira hiyo, ambapo kila shule imepangiwa kupata mipira 25 ambapo wanafunzi wataitumia wakati wa michezo.

“Ni matumaini ya Rais wetu wa TFF kuwa mipira hii inakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa, tunataka kuona vipaji vinaibuliwa kupitia mipira hii, TFF na FIFA watakuwa wanakuja kufanya ukaguzi kuona kama mipira hii inaleta tija,” amesema Kosuri.

Mwenyekiti huyo wa SIFA amemshukuru Rais wa TFF Wallace Karia kwa kuchagua Mkoa wa Simiyu kuwa miongoni mwa mikoa ya kupata mipira hiyo, ambao alieleza chama chake kitahakikisha vipaji vinaibuliwa kupitia vifaa hivyo.

Kabla ya kugawa mipira hiyo kwa shule nufaika, Mkuu wa Mkoa huo Dk, Yahya Nawanda ameishukuru TFF, ambapo ameagiza kila shule ambayo imepokea mipira kuhakikisha inatumika kwa watu sahihi.

“ Sitegemei kuona au kusikia mipira hii inatumiwa na watu wazima, hii mipira imetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi, darasa la kwanza hadi saba, tunataka kuona Mkoa wa Simiyu tunatoa akina Samatta wengi,” amesema Dk Nawanda.

Mwenyekiti wa soka la vijana mkoa Kajanja Mgengele, mipira hiyo imekuja katika wakati mwafaka, kwani FIFA na TFF wamedhamilia kuibua vipaji kuanzia ngazi za chini.

“ Kwa Mwenyekiti wa eneo hili, tuna uhakika kupitia mipira hii, tutakwenda kuibu vipaji halisi, ukosefu wa mipira ilikuwa changamoto kubwa, tunashukuru TFF na FIFA kwa kutatua changamoto hii, Amesema Kajanja.