MARA : TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imebainisha kuwa hakukuwa na ukiukwaji wowote wa haki za binadamu uliofanywa na mgodi wa dhahabu wa North Mara wakati wa zoezi la upanuzi wa eneo la uchimbaji katika vijiji vya Komarera na Kewanja wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Katika ripoti ya THBUB iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ambayo inapatikana katika tovuti yake, tume hiyo imesema kwamba katika uchunguzi wake kuhusu malalamiko dhidi ya North Mara Gold Mine imegundua kuwa mgodi huo ulitwaa ardhi yenye ukubwa wa ekari 652 katika kijiji cha Komarera kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za uchimbaji dhahabu.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba zoezi la uthamini na utwaaji wa eneo husika lilifuata taratibu na lilifanyika kwa uwazi na ushirikishwaji wa pande zote, na pia wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa walilipwa fidia stahiki.
“Katika uchunguzi kuhusu malalamiko ya wananchi wa vijiji vya Komarera na Kewanja dhidi ya mgodi wa North Mara, THBUB imebaini kwamba mgodi wa North Mara ulifuata taratibu na zoezi la utwaaji ardhi lilifanyika kwa uwazi na ushirikishwaji wa pande zote, na wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa walilipwa fidia stahiki” imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu.
Jaji Mwaimu amesema, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ililazimika kufanya uchunguzi huo na kutoa taarifa kufuatia malalamiko dhidi ya mgodi wa North Mara ukidaiwa kutozingatia utaratibu wa utwaaji wa ardhi mwaka 2021 na 2022, yaliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali MiningWatch Canada katika ripoti yake iliyotolewa Desemba 2023 likidai kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara ulioko wilayani Tarime mkoani Mara.
Katika taarifa iliyotolewa na mmoja wa maofisa wa MiningWatch Catherine Coumans na kuchapishwa kwenye tovuti ya shirika hilo, ilidai kwamba maelfu ya watu wa jamii ya wakurya wamehamishwa kwa nguvu kutoka katika ardhi yao ili kupisha upanuzi wa mgodi.
Taarifa hiyo ilidai kwamba watu wengi walihamishwa mnamo Desemba 2022, huku baadhi ya familia zikipoteza nyumba zao na ardhi mnamo Agosti na Septemba 2023.
Hata hivyo kampuni ya Barrick Gold imejibu tuhuma hizo kupitia taarifa ya Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Mark Bristow ikieleza kwamba tuhuma hizo zimetolewa kwa nia ovu na hazina msingi wowote kwa sababu zilishajibiwa kwa kina kupitia taarifa mbalimbali za mgodi wa North Mara kuhusu masuala yote yanayohusiana na shughuli za uchimbaji.
Aidha taarifa ya Barrick Gold ambayo pia inapatikana kwenye tovuti ya kampuni hiyo imesema kwamba inajivunia kazi ambayo inafanywa na North Mara Gold Mine Limited (NMGML) ya kujenga uhusiano na kuaminika katika jamii inayoishi kuzunguka mgodi huo.
“NMGML inafanya kazi na kushirikiana na mashirika mengi ya kiraia ya ndani na ya nje, kwa sera ya milango wazi na hufanya ziara na mikutano angalau kila robo mwaka, ikiwa ni pamoja na miradi maalum, kama vile mapitio ya mifumo ya malalamiko na uhamasishaji, au elimu na uhamasishaji kwenye jamii” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
North Mara Gold Mine Limited, ni mgodi wa dhahabu unaomilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation ambapo mbali na gawio la faida inayotokana na mauzo ya dhahabu, Tanzania hunufaika na kodi na tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za uchimbaji dhahabu.
Aidha manufaa mengine ya moja kwa moja yanayotokana na shughuli za mgodi huo ni pamoja na kampuni mbalimbali zinazomilikiwa na wazawa kushiriki katika mnyororo wa thamani kwa kuuza bidhaa na kutoa huduma mbalimbali mgodini hapo kupitia mfumo unaolenga kuwawezesha watanzania kunufaika na sekta ya madini maarufu kama “Local Content”
Mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) pia ni miongoni mwa manufaa wanayoyapata wananchi wa Tanzania kutoka katika mgodi huo wa North Mara Gold Mine ambao hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kugharimia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mathalani takwimu zinaonyesha kwamba kwa mwaka 2023 pekee mgodi wa Barrick North Mara ulitumia zaidi ya shilingi bilioni 7 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Tarime Vijijini.
SOMA : RC Mara aonya wanaokwamisha upanuzi wa mgodi
Aidha kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa North Mara Gold Mine Limited, Apolnary Lyambiko, mwaka huu wa 2024 mgodi huo unatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 9 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime Vijijini kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).