THRDC: Watu 1,605 wauawa kisa kimahusiano

DAR ES SALAAM: MASHIRIKA wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) yamesema watu 1,605 wameuawa nchini kutokana na migogoro ya kimahusiano katika kipindi cha mwaka 2024 hadi Juni 2026, huku wanawake na watoto wakitajwa kuwa miongoni mwa waathirika wa vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na wanachama wa mtandao huo leo, Oktoba 22, 2026, takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa matukio 941 ya mauaji yaliripotiwa nchini kuanzia Januari hadi Juni 2026, ikilinganishwa na matukio 926 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Waraka huo unaeleza kuwa kati ya matukio 941 ya mauaji yaliyoripotiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, matukio 458 yalihusishwa na migogoro ya kimahusiano.

Aidha, mwaka 2024 yaliripotiwa matukio 2,193 ya mauaji, ambapo 422 yalihusishwa na migogoro hiyo. Mwaka 2025, matukio 1,977 ya mauaji yaliripotiwa, yakiwemo 725 yaliyotokana na migogoro ya kimahusiano.

THRDC imesema mauaji hayo yanachochewa na sababu mbalimbali, zikiwemo wivu wa kimapenzi, migogoro ya ndoa na familia, madai ya usaliti, tofauti za kifedha na changamoto zinazohusu malezi ya watoto.

Katika waraka huo, mtandao umetaja matukio kadhaa yaliyoripotiwa kati ya Julai na Oktoba 2026, yakiwemo mauaji ya Leah Mazengo wa Bahi, Dodoma, na Margeth Hamis Richard wa Musoma, mkoani Mara. Pia, umetaja matukio mengine yaliyohusisha wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali nchini.

Mtandao huo umeeleza kuwa watoto wamekuwa waathirika wa moja kwa moja wa migogoro ya kimahusiano, ikiwemo kushambuliwa na kuuawa. Miongoni mwa matukio yaliyotajwa ni la watoto wawili, msichana wa miaka minane na mvulana wa miaka 10, waliouawa na baba yao mkoani Morogoro kabla ya baba huyo kujiua.

Kwa mujibu wa THRDC, ongezeko la matukio hayo linachangiwa pia na udhaifu wa mifumo ya kuzuia ukatili, ukosefu wa elimu kuhusu mahusiano salama, changamoto za afya ya akili, pamoja na upungufu wa wataalamu wa ustawi wa jamii na huduma za ushauri nasaha.

Waraka huo umebainisha kuwa baadhi ya mauaji hutokea baada ya viashiria vya ukatili kuwapo kwa muda mrefu, vikiwemo vitisho vya kuua, vipigo vya mara kwa mara, kumdhibiti mwenza na unyanyasaji wa kisaikolojia.

Kutokana na hali hiyo, THRDC imeitaka Serikali kuimarisha mifumo ya kupokea na kufuatilia taarifa za vitisho, kuongeza idadi ya maafisa ustawi wa jamii na kuweka mifumo madhubuti ya kuwalinda watu walio katika hatari ya kufanyiwa ukatili.

Pia, mtandao huo umelitaka Bunge kutunga sheria mahsusi ya kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani. Vilevile, umeziomba taasisi za elimu, viongozi wa dini, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla kuimarisha elimu kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia za amani.

Katika kuendeleza mapambano dhidi ya mauaji hayo, THRDC kwa kushirikiana na mashirika mengine ya utetezi wa haki za binadamu imetangaza kuanzisha kampeni endelevu yenye kaulimbiu “Mapenzi Siyo Vita; USIUE”, inayolenga kuhamasisha jamii kukataa ukatili na kuheshimu haki ya kila mtu kuishi na kufanya maamuzi kuhusu mahusiano yake.

Mtandao huo umesisitiza kuwa hakuna sababu ya kimapenzi inayoweza kuhalalisha mauaji, ukieleza kuwa mahusiano yanaposhindikana, wahusika wanapaswa kutafuta suluhisho la amani au kuachana bila kutumia vitendo vya ukatili.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button