Tiba utalii yaongezeka, yaingiza Sh Bil 116

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi wa Diplomasia kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi John Ulanga amesema kumekuwa na ongezeko la utalii tiba kwa asilimia 19 ambao imeongeza pato la taifa cha kiasi cha Sh Bilioni 166.5
Amesema kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 idadi ya wagonjwa waliokuja kutibiwa ndani ya nchi imeongezeka mara mbili kutoka 5,700 hadi 12,180
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Mdahalo wa wazi wa kitaalmu kuhusu utalii tiba nchini uliofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Balozi Ulanga amesemawagonjwa wanaowapokea wanatoka nchi 16 za Afrika ambapo 2,770 wanatoka Comoro, asilimia 46 wanatoka Burundi, asilimia nane Zambia,asilimia 10 DRC na asilimia nne nchini Kenya.
“Kuanzia 2021 hadi 2025 kumekuwa na ukuaji mkubwa katika huduma kama JKCI,MOI,Muhimbili,Benjamini Mkapa na Ocean Road tulikuwa tuna lengo la kupunguza watanzania wanaokwenda nje ila sasa tunavutia wagonjwa kuja ndani,”ameeleza.
Amesema ifikapo mwaka 2030 wanategemea kuwa na watalii wa matibabu 30,000 ,mwaka 2040 wagonjwa 68,000 na mwaka 2050 ambayo ndio mwisho wa dira watakuwa na wagonjwa 120,000 watakuja kutibiwa katika huduma za kibingwa.
“Mchango wa uchumi kuna mapato ya moja kwa moja kwa sasa mwaka 2025 mchango wa tiba utalii ni dola milioni 65 kwa mwaka mwaka 2030 tuna uwezo wa kufika dola milioni 200 mwaka 2040 inaweza kuwa dola 420 na mwaka 2050 itakuwa dola milioni 850,”amesisitiza Balozi Ulanga.
Mgeni Rasmi katika Mdahalo huo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema mafanikio haya yanatokana na mipango mikakati ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali .
Amesema lengo ni kutaka kufika uchumi wa kati na kutaka kuwa kitovu cha tiba utalii Afrika.

“Wizara imeandaa mazingira hadi kufanikisha tiba utalii tumeandaa muongozo wa tiba utalii na sio serikali tu hata sekta nyingine ,wizara itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wataalamu kupitia Samia Scholarship mwaka huu ipo tunategemea wataalamu katika hizi taasisi watakuwepo,”amesema Dk Shekalaghe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema asilimia 99 ya wagonjwa wa moyo sasa wanatibiwa ndani ya nchi ambapo kiasi cha Sh bilioni 95 kimeokolewa kwenda nje.
“Hadi sasa tumefikia mikoa 23 katika programu ya Samia Suluhu Hassan Outreach, ambapo wananchi wengi wamepata huduma na tumefungua hospitali Mikocheni, Kawe na Arusha tumeingia makubaliano na Seliani kutibu wagonjwa wa moyo na hivi sasa tunaenda Chato,” ameeleza.
Amesema hadi sasa wamefanya upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa 14,000,upasuaji mkubwa na mdogo kwa wagonjwa 6,000 na wagonjwa wa nje (OPD) ni 900,000.

Amesema wiki mbili zijazo wanaenda kuanza programu ya kutibu wagonjwa wa shikizo la damu iliyoshindikana.
“Tutaendelea kupanua huduma zetu tutaanzisha hospitali ya moyo Comoro na kule Mloganzila tunaanza kujenga hospitali ya moyo ya watoto,”amesisitiza Dk Kisenge.



