TIC waagizwa kulinda wawekezaji

MANYARA: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ametoa maagizo kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwalinda wawekezaji hususani wa ndani ya nchi ili wasikwame katika suala la uwekezaji huku akiwaasa pia kuwawezesha pale panapostahili ili kukuza sekta ya uwekezaji nchini.
Prof Mkumbo ametoa maagizo hayo hii leo Jumapili Januari 5, 2025 alipotembelea kiwanda cha Mati Super brands Ltd kilichopo mkoani Manyara kinachomilikiwa na mwekezaji mtanzania David Mulokozi.

Amewataka TIC kuwatazama wawekezaji kwa jicho la kipekee na kuhakikisha hawakwami kwa namna yoyote ile katika kufanikisha shughuli zao za kiuwekezaji.
“Niwaelekeze TIC wawekezaji kama hawa muwape jicho la pekee uwekezaji wao usikwame hata dakika moja,”amesema prof Mkumbo.

Aidha, katika hatua nyingine Prof Mkumbo amewataka TIC, kuwawezesha wawekezaji kwa namna yoyote ile ili kuhakikisha wanafanikisha uwekezaji wao na kuliingizia taifa kipato huku akihaidi serikali kuhakikisha mazingira wezeshi kwa wawekezaji nchini na kuahidi kuwasikiliza pindi wanapokutana na changamoto mbalimbali.
“kile ambacho wanachotaka kufanikisha tuwawezeshe wafanikiwe na tuwahaidi sisi kama serikali kuendelea kuwekeza mazingira wezeshi kwa wawekezaji hapa nchini,”amesema prof Mkumbo.
Prof Mkumbo amehitimisha rasmi ziara yake hii leo Januari 5, 2025 mkoani Manyara ambapo ametembelea kiwanda cha uzalishaji bidhaa changamshi(vileo) cha Mati Super brands Ltd kinachomilikiwa na mwekezaji wa ndani David Mulokozi ambapo kitila ametumia nafasi hiyo kumpongeza kwa uwekezaji huo mkubwa na kuahidi serikali kushirikiana naye kwa ukaribu



