TIC yahimiza wawekezaji kusajili miradi yao

KITUO cha uwekezaji Tanzania (TIC) kimetangaza kuvutiwa namna watanzania wanavyoendelea kutumia fursa za uwekezaji nchini na kimewataka wasijicheleweshe kusajili miradi yao ili kuiwezesha kupata usaidizi unaotakiwa.

Usaidizi huo ni pamoja na upatikanaji wa vyeti, leseni, vibali na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi.

Wito huo umetolewa na Meneja wa TIC Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Deusdedith Hokororo alipotembelea kiwanda cha maziwa cha Shafa Agro kilichopo katika kijiji cha Kidamali, kata ya Nzihi wilayani Iringa.

Akizungumza baada ya kutembelea na kuona ufugaji wa ngombe na uzalishaji wa maziwa unaofanywa na kampuni hiyo kubwa inayomilikiwa na mwekezaji mzawa, Hokororo amesema serikali ya awamu ya sita imeweka mkazo katika kuunga mkono uwekezaji wa ndani.

“Hiki tulichokiona hapa ndio mwelekeo wa serikali yetu katika kukuza uwekezaji hasa wa wazawa ambapo tunawahimiza kusajili miradi yao TIC ili waweze kunufaika na urahisi wa ufanyaji biashara kwa kutambulika na kituo cha uwekezaji Tanzania,” amesema.

Akizungumzia uwekezaji katika mnyoyoro wa uchumi wa nchini, amesema TIC imeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wazawa yanayowasaidia na kuwaunganisha na taasisi nyingine za serikali kwa muda mfupi ili kurahisisha shughuli zao za biashara.

Hokororo amesisitiza kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kinaendelea kuunga mkono maono ya serikali ya awamu ya sita katika kukuza uwekezaji kikilenga hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu kiwe kimesajili miradi 1000 kutoka 504 ya mwaka jana.

Kwa upande wake Meneja Uzalishaji na Ubora wa Shafa Agro, Tumaini Fredrick amesema sera na sheria rafiki za serikali zimesaidia kiwanda hicho cha maziwa kuanza uzalishaji ndani ya muda mfupi ambapo sasa bidhaa zao zinauzwa nchi nzima.

Amesema uwekezaji wa kiwanda hicho umetoa ajira za kudumu 417 mpaka sasa pamoja na ajira za muda mfupi zaidi ya 1000 kupitia uzalisha wa maziwa na vyakula vya mifugo.

Kituo cha uwekezaji Tanzania TIC kimefanya ziara katika kiwanda hicho ikiwa ni mwendelezo wa kampeni yake ya kitaifa inayohamasisha uwekezaji wa ndani ambapo tayari kimewafikia wawekezaji wazawa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Geita, Tabora, Dodoma,Singida, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga na Tanga.

Habari Zifananazo

Back to top button