TIC yasajili miradi 16 ya bilioni 1/- Shinyanga

MWENYEKITI wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC ) Binilith Mahenge ameeleza Mkoa wa Shinyanga umekuwa ukifanya vizuri katika suala la uwekezaji ikiwa tayari mwaka 2024 imeweza kusajili miradi 16 yenye thamani ya Sh bilioni 1.1.
Mahenge amesema hayo leo alipotembelea kiwanda cha kuchakata zao la pamba na kukamua mafuta cha Jielong Holdings (T) limited kilichopo eneo la N’heleghani Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.
Mahenge amesema kuwa Shinyanga ipo kwenye nafasi 10 katika uwekezaji kwa 2024 na utaratibu ulivyowekwa na Rais baada ya maboresho kufanyika karibu taasisi zote zimewekwa pamoja ili kuwarahisishia wawekezaji.
“Nimesikia hapa Shinyanga kuna maeneo yaliyotengwa kwaajili ya uwekezaji tutahakikisha tunahamasisha ili waje wawekeze na kiwanda hiki tumeona changamoto ni malighafi tutawashauri wakulima waongeze bidii ya kilimo cha pamba ili kiwanda kisisimame kwaajili ya kukosa malighafi”amesema Mahenge.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Annamringi Macha wakati ameelezea hali halisi ya uwekezaji mkoani humo alisema waliowekeza kwenye viwanda wako wengi ila baadhi wamekuwa wakichukua maeneo bila kuyaendeleleza kwa muda mrefu na wakati mwingine kuyafugia mifugo.
Ofisa biashara Mkoa wa Shinyanga Rose Tungu amesema maeneo yapo mengi ya uwekezaji yanasifa zote na miundombinu yote ipo hivyo wanakaribishwa kwenye uwekezaji na hiki kiwanda kukosa malighafi wanawashauri wakulima walime sana zao la pamba soko lipo.
Kwa niaba ya Msemaji wa Kiwanda cha Jielong Khadija Yusuph ameeleza kilianzishwa mwaka 2012 tangu kipindi hicho wamewekeza Dola za milioni 32 na kuajiri watu 30 na vibarua zaidi ya 200.

“Kiwanda kimekuwa kikisimama mara kwa mara kwa kukosa malighafi ambapo kwa sasa kinauwezo wa kutumia tani 150,000 za mbegu za pamba na upande wa jineri zimefungwa mashine 24 zinazokamua mbegu kwaajili ya mafuta”alisema Yusuph.
Mfanyakazi wa kiwanda hicho Hassan Manubi ambaye ni opareta amesema amenufaika kupata ajira na kuendesha maisha kwenye familia zao kwani changamoto kuendesha kiwanda na muda mwingine kukaa nyumbani miezi mitatu hadi mitano kwa kukosa malighafi.



