Timu 120 Iringa kuwania Mil15/- Vunjabei Cup

MASHINDANO makubwa ya Vunjabei Cup yanatarajiwa kutimua vumbi Januari 11 mkoani Iringa yakishirikisha timu 120 kutoka kila kona ya mkoa huo.
Mashindano haya, ambayo awali yalifahamika kama Ngajilo Cup, sasa yameboreshwa kwa kiwango kikubwa, ambapo zawadi ya mshindi wa kwanza imeongezwa kutoka ng’ombe mmoja hadi shilingi milioni 10.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mashindano hayo, Mratibu wa mashindano hayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo, alisema wameongeza zawadi kwa mshindi wa pili na wa tatu kutoka seti ya vifaa vya michezo hadi Sh Milioni tatu kwa mshindi wa pili na Sh Milioni mbili kwa mshindi wa tatu.
Ngajiro ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Vunjabei alisema lengo la mashindano haya ni kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi na kuimarisha mshikamano miongoni mwa jamii.
“Mashindano haya yamekuwa fursa muhimu kwa vijana kuonyesha uwezo wao kwenye soka, lakini pia ni jukwaa la kuwaunganisha watu wa mkoa wa Iringa kwa pamoja. Mwaka huu tumejipanga vyema kuhakikisha mashindano yanakuwa bora zaidi,” alisema Ngajilo.
Alisema wamepokea maombi kutoka kwa timu nyingi, lakini wamefanikiwa kupata timu 120 zinazowakilisha wilaya zote za mkoa wa Iringa,.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Iringa, Yahya Mpelembwa, mashindano hayo yatachezwa kwa mfumo wa mtoano katika viwanja viwili vikuu vya Manispaa ya Iringa na Iringa Vijijini.
Huku mashabiki wa soka wakitarajiwa kushuhudia burudani kali ya kandanda alisema mechi za kwanza zitaanza kutimua vumbi Januari 11 katika viwanja mbalimbali vitakavyotangazwa baadae.
Mpelembwa alisema timu 50 zitakazofuzu hatua ya mwanzo ya mtoano zitapatiwa vifaa mbalimbali kama jezi na vifaa vingine vya michezo ili kuongeza morali ya wachezaji.
Alisema mashindano hayo yanayofadhiliwa na kampuni ya Vunjabei yanatarajiwa kudumu kwa miezi mitatu, huku yakiwa na ratiba maalum inayotoa nafasi ya kila timu kupambana kwa haki na nidhamu ya hali ya juu.
“Mashindano haya ni ushahidi wa jinsi soka linavyoendelea kuwa chombo muhimu cha kuibua vipaji vya vijana na kuboresha maisha yao,” alisema.
Alisema kwa zawadi kubwa ya fedha taslimu na vifaa vya michezo, Vunjabei Cup inatarajiwa kubadilisha historia ya mashindano ya soka mkoani Iringa na kuweka viwango vipya vya ubora.
“Mashabiki wa soka wanahamasishwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hizi zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa na burudani ya hali ya juu, huku zikitoa nafasi kwa wachezaji chipukizi kufikia ndoto zao,” alisema.


