TIRA, Wadau wakabidhi mil 321/- Mapinduzi Zanzibar

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na wadau wake wamekabidhi hundi ya mfano ya shilingi milioni 321 kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ikiwa ni mwitikio wa Sekta ya Bima nchini kuunga mkono Maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kilele cha maadhimisho hayo kitakua Januari 12 kwenye uwanja wa Gombani, Pemba.

Akipokea hundi hiyo Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameishukuru sekta ya bima kwa hatua hiyo akisema mchango huo ni mkubwa na wanauthamini.
SOMA: Rais Mwinyi afungua Skuli ya Sekondari Tumbatu
Ameongeza kuwa fedha zilizochangwa zitatumika kama ilivyokusudiwa akihimiza sekta ya bima kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na kwamba Serikali kupitia TIRA itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watoa huduma za bima.
“Natoa wito kwa kampuni za bima nchini kuchangamkia fursa za Biashara zilizopo kupitia miradi inayoendelea Zanzibar na ofisi yangu ipo tayari kutoa msaada pale inapohitajika,” amesema Abdulla.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Bima Tanzania, Khadija Said akiongoza ujumbe uliokabidhi hundi hiyo ameeleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya sekta ya bima nchini ya kuwa sehemu ya maadhimisho hayo ili kuibua na kuchochea ushirikiano wenye tija na Serikali hususan kwenye miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini kuona namna kampuni za bima zinavyoweza kushiriki kwenye kukinga majanga.
Mwakilishi wa Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI) Wilson Mnzava ambae pia ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya CRDB (CIC) ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikisha Kampuni za Bima katika tukio hilo muhimu
“Huu ni mwanzo tu tunaahidi kwamba tutaendelea kushiriki kila mwaka ili kuhakikisha kwamba sekta ya bima nchini inakuwa ni miongoni mwa mafanikio ya maadhimisho haya,” amesema Mnzava.
Aidha, Mnzava ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kutoa fursa kwa kampuni za bima za nchini ili ziweze kushiriki kwenye kukinga miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa chini ya serikali na wawekezaji binafsi.