TMA yatoa tahadhari kwa wakulima,wafugaji

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa maangalizo kwa sekta nyeti nchini ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi na usafirishaji, kufuatia utabiri wa msimu wa mvua za chini ya wastani hadi wastani unaotarajiwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora.
Akizungumza na maafisa utumishi wa Idara ya Kilimo na TMA mkoani Tabora, Meneja wa TMA Kanda ya Magharibi, Waziri Waziri, amesema mwenendo huo wa mvua unaweza kusababisha upungufu wa unyevu kwenye udongo na hivyo kuathiri ukuaji na maendeleo ya mimea, jambo litakaloweza kupunguza mavuno hasa kwa mazao yanayategemea mvua.

Aidha, amesema sekta ya mifugo na uvuvi pia zinaweza kukumbwa na changamoto ya upungufu wa maji na malisho, hali inayoweza kuchochea migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. SOMA: Watengeneza mfumo kudhibiti hali ya hewa mashambani
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk. John Mboya, ametoa wito kwa maafisa ugani na wataalamu wa kilimo kuhakikisha wanawafikia wakulima moja kwa moja kupitia mikutano ya vijiji na kata, ili kuwapatia elimu na taarifa sahihi kuhusu mwenendo wa hali ya hewa.
Katika hatua nyingine, TMA imesisitiza kuwa uelewa na maandalizi ya pamoja kati ya serikali, wataalamu na wananchi ni nguzo muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.



