TPA Mtwara wapokea meli sita kusafirisha korosho

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) mkoani Mtwara mpaka sasa imepokea meli sita za makasha matupu kwa ajili ya kusafirisha korosho ghafi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025.

Akizungumza wakati uongozi wa mkoa huo ulipotembelea bandarini hapo kwa lengo la kujionea utayari wa bandari katika kuhudumia msimu huo wa korosho, Kaimu Meneja wa Bandari hiyo, Sudi Mtunze amesema hadi sasa tayari wameshapokea meli hizo 6 za makasha matupu.

Amesema hadi sasa jumla ya makasha 2,791 yapo tayari bandarini hapo kwa ajili ya kuwahudumia mawakala na usafirishaji wa korosho katika msimu huo.

Advertisement

Hata hivyo wanategemea kupokea meli nyingine ya makasha 900 mstupu hivyo kupelekea kuongezeka kwa idadi hiyo ya makasha yaliyopo kwa sasa.

“Kwa ufupi bandari ya mtwara tumejipanga kikamilifu kivifaa na miundombinu yote tupo tayari kuhudumia msimu wa korosho”alisema Mtunze

Amesema bandari hiyo kwa msimu huo wa korosho mwaka 2024/2025 inatarajia kusafirisha tani laki 280,000 hadi yani laki 300,000 huku msimu wa korosho uliyopita ilisafirisha tani 253,000.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema wametembelea bandarini kwa lengo la kujionea na kufatilia utayari wa bandari katika usafirishaji wa shehena mbalimbali zinazosafirishwa kupitia bandari hiyo ikiwemo korosho katika msimu huo wa mwaka 2024/2025.

Aidha maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini Rais Samia Suluhu Hassan kuwa korosho zote zinazozalishwa katika mkoa wa Mtwara, Ruvuma na Lindi zisafirishwe kupitia bandari hiyo ya mtwara.

“Kwahiyo tumekuja kuona utayari na tunashukuru wametuhakikishia kwamba wako tayari na meli zimeshaanza kuleta makasha kwa ajili ya upakiaji wa korosho hizo”amesema Sawala

“Tunayo furaha kuwahakikishia umma kwamba sisi wanamtwara lakini kwa niaba ya serikali katika mkoa wetu wa mtwara kwamba, bandari ya mtwara ipo tayari kutekeleza maelekezo ya mheshimiwa Rais wetu”

Sawala ametoa wito kwa wadau wote wanaohusika na zao hilo wakiwamo waendesha maghala wa vyama vikuu vya ushirika kuwa, korosho zinapotoka katika maghala yao wahakikishe zinaenda bandarini hapo na siyo vinginenevyo.