SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) limezindua zoezi la mwisho la uhakiki wa wananchi halali ambao maeneo yao yatachukuliwa na shirika hilo kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka eneo la uchimbaji la Ntorya kwenda kiwanda cha kuchakata gesi hiyo cha Madimba mkoani Mtwara.
Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan, leo Novemba 23 katika kijiji cha Namahyakata Kata ya Nanguruwe wilaya ya Mtwara ambapo ujenzi huo unatarajia kuanza.
Kyobya amewataka watendaji katika kata 4 na vijiji 11 ambao bomba hilo lenye urefu wa kilomita 35 litapita kuhakikisha wanafanya uhakiki wa kina wa wananchi wanaostahili kulipwa ili kuepuka migogoro ambayo inaweza kujitokeza wakati wa malipo.
“Niwaombe watendaji wa kata nne na vijiji 11 mhakikishe uhakiki unafanyika kwa kina jina kwa jina, mtu kwa mtu na sura baada ya malipo kusiwepo na changamoto ya malalamiko kwa wahusika halali,” amesema.
Aidha, Afisa Miliki Mwandamizi wa TPDC Happy Mwaseba amesema wananchi 253 kutoka kata nne na vijiji 11 wanatarajia kulipwa fidia kupisha ujenzi wa bomba hilo ambalo la litasafirisha gesi asilia kutoka eneo la uchimbaji la Ntorya kwenda kwenye kiwanda cha uchakataji wa gesi hiyo cha Madimba Mkoani Mtwara.