TRA kutumia ‘Ndondo Cup’ kuzuia utumiaji bidhaa hatarishi
DAR ES SALAAM: MKURUGENZI wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema TRA imeamua kutumia michezo katika kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhakiki bidhaa kabla ya kuzitumia ili kuhakikisha kuwa ni salama, halisi na zinatii kanuni za kodi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kayombo amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeingia udhamini wa Sh milioni 40.5 kwenye mashindano ya Ndondo Cup, kwa kushirikiana na Uongozi wa Michezo wa Shadaka. Udhamini huu muhimu unaashiria dhamira ya TRA ya kukuza ushirikishwaji wa jamii kupitia michezo huku ikikuza mipango muhimu ya elimu ya kodi.
“Kupitia michezo, tunaweza kufikia hadhira kubwa zaidi ili kuwaelimisha na kuwashawishi kufahamu suluhisho la kisasa zaidi la Stempu za Ushuru za Kielektroniki (ETS) katika kuhakikisha uhalisi wa bidhaa. Zaidi ya hayo, tunaamini kuwa kupitia mpango huu, tunaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa tabia za watumiaji na kuchangia katika lengo pana la kuimarisha uzingatiaji wa kodi kote nchini,” ameeleza mkurugenzi huyo.
Amesema, TRA kwa kushirikiana na kampuni ya SICPA, ambaye ni mshirika mkuu wa teknolojia wa Stempu za Kielektroniki za Ushuru za TRA, itatumia jukwaa la Ndondo Cup kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu ETS na kampeni ya Hakiki Stampu.
TRA inatoa wito kwa watumiaji wa bidhaa zenye Stempu za Ushuru za Kielektroniki (ETS) kupakua programu ya Uthibitishaji wa Stempu na kuhakiki bidhaa hizo kabla ya kuzitumia. Hii ni njia mojawapo ya kulinda afya zao na kuhakikisha serikali inapata mapato sahihi ya kodi.
Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Usimamizi wa Michezo wa Shadaka, Shaffih Dauda, ameishukuru TRA katika kuongeza thamani ya michezo ya ndani.
“Tunafuraha kuwa na TRA kama wadhamini wakuu wa Ndondo Cup mwaka huu. Udhamini huu sio tu kwamba unasaidia maendeleo ya soka la chini lakini pia una lengo kubwa zaidi kwa kuelimisha umma juu ya masuala muhimu ya kodi, vilevile viwanja vyetu vya michezo vinajaa bidhaa mbalimbali, hivyo tunatarajia ushirikiano huu ili kuhakikisha teknolojia hii inasaidia. tujikinge na bidhaa feki kwa tunapokuwa viwanjani,” amesema Dauda.
Ndondo Cup imekuwa ikiadhimishwa kwa muda mrefu kwa namna inavyokuza vipaji vya soka vya ndani na kuleta jamii pamoja. Kwa msaada wa TRA, mashindano ya mwaka huu yanapangwa sio tu kuburudisha bali pia kuelimisha umma kuhusu masuala muhimu yanayohusiana na kodi, kuhimizia umuhimu wa kufuata sheria na manufaa ya mfumo wa Stampu za Kielektroniki za Ushuru na Hakiki Stempu.