TRA kuwaongezea faida wafanyabiashara
MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) imeweka wazi kuwa itajikita zaidi katika mfumo shirikishi na elimu kwa mlipa kodi ili kuwawezesha wafanyabiashara siyo tu kulipa kodi kwa wakati bali pia kuongeza faida kwenye biashara zao.
Meneja wa Elimu kwa mlipa kodi kutoka TRA, Paul Walalaze amesema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita mkoani humo.
Walalaze amesema ili kufanikisha mpango huo serikali imefanya mabadiliko ya sheria tofauti ambazo hapo awali zililalamikiwa na wafanyabiashara kuwa siyo rafiki na sasa TRA inafanya kazi kwa sheria mpya.
SOMA: Bosi TRA ato Bosi TRA atoa msimamo
“Mwaka huu tumeona sheria mbalimbali zimebadilishwa, sheria ya kodi ya mapato, sheria ya usimamizi wa kodi, sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na yenyewe imenadilishwa,” amesema Walalaze.
Amesema manufaa ya kubadilisha sheria hizo ni kuzifanya kuwa chachu ya ukuaji wa biashara na zifanyike vizuri ili faida iongezeke na TRA ikusanye kodi kwa mjibu wa sheria.
“Kwa kukaa karibu na wafanyabiashara, kuwaelimisha siyo tu sheria za kodi lakini pia tunawaelimisha mbinu za kufanya biashara ya faida,” amesisitiza Walalaze.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, Peter Sanga amekiri kuridhishwa na mabadiliko yaliyofanyika kwenye sheria za kodi nchini ili kuondoa mfumo wa kodi kandamizi.
Sanga amesema mabadiliko ya sheria yamepunguza malalamiko na migongano iliyokuwepo kati ya TRA na wafanyabiashara hususani sheria ya usimamizi wa kodi hasa kwa mfanyabiashara asipotoa risiti.
“Sheria iliyokuwepo, ukikamatwa hujatoa risiti faini yake ilikuwa shilingi milioni 15, ilikuwa ni maumivu makubwa sana kwa sisi wafanyabiashara.
“Ukiangalia kwa maeneo yetu hapa Katoro wafanyabiashara wengi bado ni wadogo, ukimpiga faini ya shilingi milioni 15 tunaita huko ni kumfilisi,” amesema Sanga
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara Katoro, Simon Kasatu ameshauri mbali na mafanikio hayo ni vyema TRA ijikite kwenye sera rafiki ambazo siyo tu zitasimamia biashara bali pia zitazalisha mabilionea wengi zaidi nchini.
View this post on Instagram